Ijumaa, 28 Machi 2014

JINSI TUNAVYOWEZA KUTUMIA MITAALA TZ KUKUZA VIPAJI NA.1

kwa kuanzia nitauzungumzia mtaala wa elimu ya secondari.Kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu mitaala ya Tanzania kwamba haikidhi matarajio ya mwanafunzi kwa maisha yake baada ya kutoka shule.
Mfano;-

1.watu wengi wamekuwa wakilalamikia kuwa mitaala iliyopo haimuandai mototo kuishi maisha ya kujitegemea baada ya kumaliza masomo yake.Wangependa mwanafunzi akimaliza sekondari awe mjasiriamali,mkulima nk.

2. Malalamiko mengine ni kuwa watoto wamekuwa wakisoma masomo mengi kupita kiasi ,Kitu kinachomfanya mwanafunzi kuwa na mzigo mkubwa wa mambo ya kujifunza.Wangependa kuona wanafunzi wanasoma masomo machache tu ili wayamudu.

3. Pia wamekuwepo watu wanaodai kuwa mambo ambayo wanafunzi Tanzania wanajifunza hayahusiani na maisha tunayoishi.Yaani wanajifunza mambo ambayo hatuyahitaji katika maisha yetu.

4. Wapo wanaodai kuwa eti elimu inayotolewa Tanzania bado ni ya kikoloni na siyo ya kiuzalishaji kama inavyokusudiwa.
5.Wapo wanaodai kuwa elimu ya ujasiriamali haijapewa kipaumbele katika elimu ya Tanzania.

6.Maswala ya kijamii nayo yamelalamikiwa kuwa eti hayajawekewa mkazo katika elimu ya tazania.Inamaanisha kuwa eti inawafanya watu wasiwe wanajua haki zao, wasiwe wawajibikaji,waadilifu,nk.

7.Michezo vivyohivyo imelalamikiwa kuwa haijatiliwa mkazo katika elimu ya Tanzania.Kwamba watoto hawajafundishwa michezo kama somo rasmi nk.

8.Hata maswala ya kilimo yamezungumzwa kutozingatiwa katika elimu ya Tanzania.Baadhi ya malalamiko yanadai kuwa wahitimu wengi hawapendi kufanya kilimo kwakuwa hawakufundishwa kilimo mashuleni.

Nitakubaliana na malalamiko hayo kwa sehemu ndogo sana .Lakini cha kushangaza ni kwamba malalamiko mengi yanatokana na kutoifahamu mitaala yenyewe.Cha ajabu zaidi ni kwamba hata watu wenye elimu wamekuwa wakiilalamikia mitaala kwamba ndiyo kikwazo cha maendeleo ya Tanzania.Kifupi ni kwamba malalamiko mengi sio ya kweli na hayatujengi,hivyo yanatunyima fursa ya kutumia mitaala iliyopo kikamilifu ili kuleta tija kwa taifa letu.

Kwa kuupitia mtaala wenyewe kwa ufupi ninaimani sote kama wadau muhimu wa elimu yetu Tanzania, tutagundua mambo mazuri na hatimaye kuyatumia kama mtaji, katika kuibua na kuboresha vipaji vya wanafunzi wetu.

(I) MAANA YA MTAALA
Wataalamu wa masuala haya wanadai kuwa mtaala una maana nyingi sana kutokana na dhana tofautitofauti . Taarifa ya TAASISI YA ELIMU YA MWAKA 2013 MARCH ya maboresho ya mitaala tangu mwaka 1961 hadi 2010,inadai kwamba dhana ya mtaala, ikijumuisha nadharia zake na muundo wake (models) ni eneo la taaluma lenye mitazamo (perspectives) tofauti.

Lakini taarifa ya taasisi hiyohiyo na mwaka 2005 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2013 ya mtaala wa elimu ya secondary iliyoandikwa kwa lugha ya kiingereza katika utangulizi wake inasema ( Curriculum is generally prescribed as a set of standards that guides the delivery of education by considering the following areas:) mtaala ni viwango vilivyopangwa au kuwekwa na serikari ili kuongoza utoaji wa elimu kwa kuzingatia maeneo yafuatayo;-

Maeneo hayo ndiyo yale yanayotajwa na taarifa ya mabadiliko ya mitaala tangu mwaka 1961-2010, iliyotolewa mwezi march 2013 nayo ni –

(i) Ujuzi watakaoujenga wanafunzi (competences) yaani maarifa (knowledge), stadi (skills) na mwelekeo (attitudes),
(ii) Njia za kufundishia na kujifunzia zitakazotumika katika utekelezaji wa mtaala (pedagogical orientations),
(iii) Vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinavyohitajika,
(iv) Upimaji, ufuatiliaji na tathmini ya mtaala husika.
(v) Sifa za kitaaluma na kitaalamu za mwalimu atakayeuwezesha mtaala husika,
(vi) Miundombinu wezeshi (enabling infrastructure) kwa utekelezaji wa mtaala wenye ufanisi,
(vii) Muda utakaotumika katika ufundishaji/utekelezaji mtaala

Ili kupata uelewa mzuri kuhusu mtaala hatuna budi kugusia pia na sera ya elimu ambayo ndiyo inayozaa mtaala.

TAMKO LA SERA YA ELIMU
Mtaala wa elimu ya sekondari nchini unatokana na kitu kinachoitwa TAMKO LA SERA YA ELIMU (EDUCATIONAL POLICY STATEMENT)

Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa tamko la sera ya elimu ni kwamba utoaji wa elimu katika nchi ni lazima uendane na matakwa au mahitaji ya nchi husika,na vilevile mahitaji au matakwa ya dunia.Mtaala umezingatia pia mazingira ya kijamii na ya kiuchumi bila kuacha upande wa pili yaani yatakayoendana na hali kama hizo kidunia.

Chukulia kuwa kama kila nchi ingeamua kufundisha watoto wa nchi husika kwa kuzingatia mahitaji ya nchi yao tu, leo dunia ingekuwa na hali gani,kiuchumi,kijamii,kisiasa,kidiplomasia ,nk ?.Lakini kwa kuzingatia matakwa ya dunia ya leo mtaalamu yeyote anaweza kuwa msaada au kufanya kazi popote kutokana na maandalizi aliyoyapata akiwa shuleni.

Swala hili linatupa ushahidi tosha kabisa kuwa kuna umuhimu wa kutazama na upande wa pili katika maswala haya ya elimu.Tusije tukatengeneza kizazi kitakachoshindwa kuendana na dunia kwa kukosa maarifa na ujuzi utakaokifanya kiwe nyuma au kutofiti kabisa katika dunia yaleo.Haya yote yanawezekana tu pale tutakapoachana na fikra za kuzalisha wachuuzi wa kwenda china na dubai kwaajili ya maisha ya tumbo na mavazi.

Matamanio ya watu wengi ni kuzalisha wachuuzi tu na sio wataalamu.Kama unandoto za kuzalisha wachuuzi basi mtaala huu hautakufaa kabisa kwa kuwa umelenga kuzalisha wataalamu .Mwanafunzi wa sekondari lazima ajengwe katika msingi imara wa nadharia ya mambo mengi ili achague machache atakayoyafanyia kazi mbele ya safari katika maisha yake.

Ni lazima mwanafunzi atengenezwe ili kujisaidia yeye mwenyewe ,jamii inayomzunguka na kuwa na mchango katika dunia.Kumbuka kufeli na kubaki nyumbani ni bahati mbaya tu.
Kama utausoma vizuri mtaala wa sekondari utagundua unaandaliwa kwa lengo la kumfanya mwanafunzi kuwa tayari kuendelea na masomo ya juu, na endapo hataendelea basi atatumia ujuzi huo mdogo kujikimu yeye mwenyewe kufuatana na juhudi alizonazo.

Tukumbuke kuwa kama tutaamua kuwavuna na kuwatumia kwa matumizi yetu basi bado watahitaji ujuzi wa ziada ili waweze kufaa kwa shughuli za kijamii.Mifano mizuri tumeiona kwa JESHI LA POLISI,JESHI LA WANANCHI, NA JESHI LA KUJENGA TAIFA,NA BAADHI YA VIWANDA NA TAASISI.Hawa huwachukuwa vijana hawa na kuwapa mafunzo maalumu na kuwatumia kwa kazi mbalimbali na ufanisi wake sote tumeushuhudia.Asilimia kubwa ya wazalishaji wa nchi hii ni vijana waliotoka katika kundi hili.

Sasa ili kujiridhisha kuwa mtaala unazingatia mambo yote muhimu tunayoyakusudia tutazame muhutasari wa malengo ya mtaala kwa ujumla wake kabla ya kuzama ndani zaidi .
MALENGO YA MTAALA WA ELIMU YA SEKONDARI TANZANIA
Mambo haya yameainishwa katika mtaala wa elimu kama ulivyoboreshwa mwaka 2013 nayo ni ;-

1.Kuimarisha na kupanua mtazamo wa mawazo ya msingi ,maarifa , ujuzi, na kanuni zilizopatikana na kuendelezwa shule za msingi.

2.Kuboresha maendeleo zaidi na kutambua umoja wa kitaifa,utambulisho,maadili,uwezo binafsi,kuheshimu na utayari wa kufanya kazi,kutambua haki za binadamu,utamaduni,utashi ,desturi,mila, majukumu ya kiraia na wajibu.

3.Kuinua maendeleo ya uwezo katika lugha na matumizi ya ufanisi ya ujuzi wa mawasiliano katika lugha ya Kiswahili na angalau moja ya lugha ya kigeni.
4.Kutoa fursa kwa mahitaji ya maarifa, ujuzi , jitihada, na uelewa katika eneo la kujifunza lilichaguliwa.

5.kumuandaa mwanafunzi kwa elimu ya ngazi ya tatu na ya juu,ya ufundi, ufundi sanifu,na mafunzo ya kitaalamu.

6.Kuamsha hisia na uwezo wa usomaji binafsi,kujiamini na kujiendeleza katika waanzilishi wapya wa sayansi na teknolojia,taaluma,ujuzi wa kikazi,na mbinu

7.Kuwaandaa wanafunzi kuingia katika dunia ya kiutendaji.

Nimelazimika kunukuu mambo hayo ya msingi kutoka katika mtaala wa elimu ya sekondari ulioboreshwa mwaka 2013 kwasababu kwa sehemu kubwa yanajibu maswali mengi ambayo yamekuwa yakiulizwa na wengi.

Utaona tofauti kubwa sana na tulikotoka mfano mwaka 1967 malengo makuu ya mtaala yalikuwa ni;-

1. Kuwafunza watoto wajione kuwa sehemu ya jamii wanazoishi.

2. Elimu kupanda mbegu ya watu kuishi pamoja na kufanya kazi pamoja.

3. Elimu iwafanye watoto kujiona wote ni sawa kibinadamu na kuondoa majivuno ya kikabila, rangi, dini na elimu.

4. Kujenga stadi za kudadisi na kujenga moyo wa kujiamini.

5. Kuandaa watoto kwa kazi za maisha ya vijijini na wanaojitegemea.

Kwa vyovyote vile pamoja na matokeo mazuri ya mitaala ya wakati huo, ambayo shabaha yake kuu ilikuwa ni kumuandaa mototo kutumia zaidi rasirimali zilizomo ndani ya eneo lake  tuu kwaajili ya kujikwamua kiuchumi,Lakini sasa mtaala unatakiwa kumuandaa mwanafunzi kutumia rasirimali zilizomo katika dunia kwaajili ya kujikwamua kiuchumi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni