Jumanne, 27 Mei 2014

MBINU ZA USHINDANI KATIKA ELIMU


Bila hata kumeza mate naweza kusema kuwa hata katika elimu kuna mbinu za kiushindani. Na ushindani huu ni ule unaopatikana ndani ya darasa na hata baada ya kuhitimu kiwango fulani cha elimu.Ndani ya darasa ni kuwa kinara kwa  kujipatia ufaulu unaoridhisha na nje ya darasa ni ule ufanisi anaokuwa nao muhitimu katika utendaji wake.

Ukosefu wa mbinu hizo unaweza kukusababishia kushindwa vibaya darasani na hata baada ya kumaliza shule au chuo.Vilevile ningependa kusema kuwa,mbinu hizi ni za ujumla na zina muhusu mtu yeyote anayesoma ngazi yeyote ya elimu iwe rasmi au si rasmi. Pia zina muhusu hata Yule anayetarajia kujiunga na elimu wakati wowote.

1.     KUWA WA KWANZA KUPATA TAARIFA ZINAZO KUHUSU


Taarifa ni muhimu kwa kila mtu.Lakini muhimu zaidi ni zile zinazo kuhusu, mfano kama wewe ni mwanamichezo basi utakuwa hufanyi busara kama kila kukicha utakuwa ukitafuta habari za siasa.Ni wazi kuwa hazitakuwa na tija sana katika uwanamichezo wako japo zitakusaidia.

Vivyo hivyo kwa mwanafunzi au kwa mwana kisomo yeyote ,unalazimika kuwa wa kwanza kupata taarifa zinazo kuhusu kuliko mtu mwingine yeyote.kufanya hivyo kutakusaidia kujua kinachoendelea katika elimu,mabadiliko mapya,fursa mpya za elimu,changamoto,na mwelekeo  wa elimu yako kwa ujumla.Taarifa hizi utazipata kupitia vyanzo vyote vya habari ikiwamo mitandao, na jamii iliyokuzunguka.

Manufaa utakayoyapata ni pamoja na ufahamu wa kutosha kuhusu elimu (awareness),kujipanga haraka kama kuna mabadiliko mapya au changamoto,kuwa wakwanza kupata fursa kama zipo,kuendana na wakati (up-to-date).Kwa sababu hiyo wewe ndiye utakaye kuwa kinara katika mkondo  wako wa elimu na  mwamuzi wa hatima ya elimu yako na si mazingira.

2.     USIRIDHIKE KUONGOZA DARASANI

Kuridhika kuongoza kundi dogo la darasa lako kunaweza kuleta matokeo mabaya sana mwisho wa safari ya elimu yako.Hapa ningeomba nitumie msemo mmoja ambao nimekuwa napenda sana kuutumia (don’t run faster to be the first but the best) usikimbie zaidi ili kuwa wakwanza bali kuwa bora kuliko wote.

Wakati mwingine katika mtiririko wako wa elimu unaweza kukutana na watu ambao uwezo wao wa kuelewa ni wa kiwango cha chini sana, hivyo kukufanya wewe kuwazidi kimatokeo kila kukicha.Kinacho kupasa kufanya ni kujipima kimatokeo na alama za juu kabisa za ufaulu hata kama umekuwa ukiwazidi  wenzako mlio kundi moja.

3.     JITAHIDI KUA BORA KULIKO KIWANGO CHA ELIMU YAKO

Hapa nina maana kuwa uelewa utakao kua nao uwe zaidi ya elimu uliyopata darasani.Elimu tunayoipata darasani hata iwe ya degree ngapi ,ni ndogo sana ukilinganisha na mahitaji makubwa ya elimu inayotakiwa katika maisha yetu.Na kwasababu hiyo ndiyo maana hata kama umesoma vipi bado kutakuwa na uhitaji wa elimu ya ziada ili kukidhi sehemu kubwa  ya mahitaji muhimu ya kimaisha.

Sasa, ili kumudu ushindani wa elimu na wewe kuwa bora kuliko ilivyo kawaida inategemea ni  jinsi gani utakavyokuwa ukijielimisha zaidi kuliko kutegemea kuelimishwa tuu darasani.

Kutofanya hivyo ndiyo kusema kuwa tutakuwa na kundi kubwa la watu wenye viwango vya juu vya elimu lakini linapokuja swala la uelewa na ufanisi kiutendaji ni kitendawili.

*Tunakua na wahitimu wengi wa darasa la saba lakini kiwango chao cha uelewa  na ufanisi kinafanana na cha  darasa la pili.
*Tunakua na wahitimu wengi wa form four lakini kiwango chao cha uelewa kinafanana na cha darasa la saba.
*Tunakua na wahitimu wengi wa kidato cha sita lakini uelewa wao na ufanisi unafanana na form two.
*Tunakua na wahitimu wengi wa vyuo lakini uelewa wao unafanana na ule ambao angekuwa nao muhitimu wa form four.

Vivyo hivyo wakati mwingine inakupa shida kusikia kuwa mtu fulani ana degree mbili na kadhalika,yaani alivyo kwa ujumla wake hafanani na kiwango cha elimu aliyonayo.Hafanani kwa jinsi anavyoamua mambo,hafanani kutokana na matokeo ya kiutendaji anayoyapata,hafanani kwa jinsi anavyojieleza,hafanani kwa jinsi anavyojitambua,wala hafanani kwa jinsi anavyochangia katika jamii.

Nashauri kuwa , jitahidi kubadilisha hali hii yaani iwe hivi:-
 kwa muhitimu wa darasa la saba ue na uelewa kama wa muhitimu wa form four na zaidi; yaani ikitokea mtu hakupata nafasi ya kukuuliza adhanie kuwa wewe ni muhitimu wa kidato cha nne au zaidi.


Kwa wale wa degree moja jijenge kiasi kitakachofanya mtu afikirie kuwa pengine  una mbili au zaidi.


form four na six angalau mtu akijichanganya ahisi kuwa labda ni muhitimu wa chuo au degree kwa jinzi ulivyojitahidi kukuza Thamani ya elimu yako kwa kujielimisha binafsi kila kukicha.


Kufanya hivyo kutakupa  Manufaa ya kuwa mtawala wa kiwango cha elimu uliyoifikia  na kama utapimwa kwa kigezo cha elimu husika, basi wewe utakuwa uko mbali kupita kiasi.Hata hivyo,hiyo ndiyo itakuwa mundu wa kutakatisha njia kuelekea mafanikio kupitia elimu uliyoipata.

4.     EPUKA DHANA POTOFU ZINAZOHUSU ELIMU

Mada hii ya dhana potofu kuhusu elimu  nimeizungumzia kirefu katika mada inayosema MBINU ZA KUEPUKA DHANA POTOFU DHIDI YA ELIMU ukipata nafasi unaweza kusoma mwenyewe.
Kifupi naweza kusema kuwa kumekuwa na dhana nyingi potofu zinazohusu elimu ambazo unahitaji kuzifahamu mapema na kuziepuka.Baadhi ya dhana hizo ni kama ifuatavyo,

       Ipo dhana inayosema kuwa wahitimu wa elimu ya sasa hawana wanacho kielewa hivyo hawana tija kwa jamii.Kitu ambacho si kweli kwasababu ushahidi umeonyesha kuwa darasa la saba,form four na six wote wamefanya vizuri  jeshini,polisi ,magereza,viwandani,super markets,mashanbani,kwenye biashara ndogo na kati na maeneo mengine kwa kupata mafunzo kidogo tu ya kuwawezesha kumudu shughuli zao.Tena cha kushangaza zaidi wengine wamemudu bila hata mafunzo yeyote ya ziada.

2       Kuna dhana kuwa wahitimu wa vyuo wengi hawana uwezo katika uzalishaji.Wakati dhana hii ikiendelea kukuzwa ndiyo kwanza hivi sasa kigezo kikubwa katika soko la ajira za maofisini ni angalau degree moja.Hii inaonyesha kuwa sio kweli kwamba hawana uwezo bali wengi wao wanzagaa mtaani na pale wasipo hitajika kwa kukusa cha kufanya.

3       Ipo dhana kuwa ukisoma sana hutapata kazi .Dhana hii imewafanya watu wengi kuvunjika moyo wa kuweka mikakati ya elimu ya kufika mbali kwa kudhani kuwa haitawasaidia sana,eti kwamba ukisoma sana waajiri watakuogopa.

      Dhana hii sio kweli kwa kuwa ushahidi umeonyesha kuwa waliosoma sana ndiyo wenye fursa kubwa zaidi katika soko la ajira.Vivyo hivyo hata katika swala zima la  ufanisi wa kazi ,mtu mwenye elimu kubwa zaidi ndiye mwenye ufanisi mkubwa zaidi katika utendaji.

Hii iko hivi; mtu mwenye kiwango kidogo cha elimu namfananisha na mashine yenye nyenzo chache na zisizo na ubora; inayotumia nguvu nyingi na kupata matokeo kidogo.Mfano inaweza kuwa ni mashine inayo tumia mafuta mengi ,inafanya kazi taratibu na ubora wa kazi ni hafifu. Mtu  mwenye kiwango kikubwa cha elimu namfananisha na mashine iliyoboreshwa na kuwekewa nyenzo nyingi zinazoweza kufanya kazi haraka na kwa urahisi na kwa kiwango cha hali ya juu, hivyo kuleta matokeo makubwa.

 Hilo unaweza ukaliona  mahospitalini kwa madaktari bingwa,kwa watafiti wa kilimo,wanafalsafa,saikolojia,wanasheria,mainjinia,wahadhili vyuoni nk.


Sio lazima kuwa ukisoma basi utalazimika kuajiriwa,bali unaweza kuitumia fursa ya elimu uliyoipata kwa kutengeneza ajira binafsi na za wengine.
Kuna dhana nyingine nyingi potofu ambazo zinaweza kukuvunja morali wa kutafuta elimu zaidi ambazo isingekuwa rahisi kuzitaja hapa, bila shaka utazisoma katika mada husika .

5.     EPUKA KUFIKIRI KUJA KUWA NANI BALI KUFANYA NINI.

Jiepushe kabisa na fikra za kizamani za kuja kuwa waziri,mbunge,meneja katika maofisi makubwa,na vitu vinavyofanana na ubosi ubosi.Ondoa fikirani mwako taswira za kimwonekano  bali za kiutendaji. Kumbuka hatusomi ili tuje kuwa nani bali kuja kufanya nini.sahau kuhusu kuwa mwalimu bali  kufundisha,sahau kuhusu kuja kuwa daktari bali kutibu watu,sahau kuhusu kuja kuwa afisa kilimo bali kulima,sahau kuhusu kuja kuwa meneja biashara bali kufanya biashara nk.Ili uwe na ushindani wa kutosha katika elimu ni pale unapo jidhatiti kuja kufanya nini baada ya kuhitimu masomo yako.

Kitendo cha  kufikiri kufanya nini na si kuja kuwa nani kitakuongezea bidii ya kujifunza na kujijengea uwezo binafsi juu ya kile unachojifunza.Kumbuka nafasi yako ya kujifunza ni ile unapokuwa darasa na  baada ya kuhitimu kinachofuata ni uzalishaji.Na wajibu wa kuzalisha utakuwa ni wako wala si wa mtu mwingine.

6.     FAHAMU KUHUSU NGAZI YA ELIMU INAYOFUATA

      1.       JIFAHAMISHE KUHUSU UTAKACHOTAKIWA KUJIFUNZA  BAADA YA UNACHOJIFUNZA SASA
     kitendo hicho kitakusaidia kukupa mwanga wa kule unakokwenda kitaaluma na kukupa ufahamu wa ziada juu ya unachosoma.Utakapofika kujifunza itakuwa sawa na mtu anayefanya safari ya kurudi yaani si mgeni tena na anachofundishwa.


      2.       PATA TAARIFA WAPI INAPATIKANA ELIMU UNAYOITAKA
      Hapa ni pamoja na kuhudhuria makongamano ya elimu,kutafuta taarifa kutoka vyuoni na kwingineko.
      Ni ajabu iliyoje kuona mtu anamaliza kidato cha sita hajui  asome kozi gani,chuo gani,na kwa sifa gani.Vivyo hivyo kwa darasa la saba, zifahamu shule zinazotoa elimu ya sekondari na mahali ziliko na mahali pengine panapotoa elimu kama hiyo.

kwa wanafunzi wa kidato cha nne ni lazima ujiweke tayari kujua shule zinazotoa elimu ya A’level, vyuo vinavyotoa kozi mbalimbali , sifa za kujiunga ikiwamo kozi zinazotolewa.Sio busara kudhani kuwa unaweza  kuja kusoma kozi yeyote tuu, kitu ambacho kitakufanya kujiingiza katika kozi zisizoendana na kipaji chako. Ili kujielimisha zaidikuhusu swala hili unaweza ku bofya mada hii JINZI YA KUTAMBUA KIPAJI CHAKO.


kwa wale watu wa vyuo ni muhimu kujifahamisha mapema ni kozi gani zitakazo kufaa baadaye na zinapatikanaje kwa hatua inayofuata.

      3.       PATA TAARIFA YA SOKO LA AJIRA KABLA HUJAJIUNGA NA KOZI
            Utafiti juu ya soko la ajira ni muhimu na hii itakusaidia kujua changamoto zilizopo na kama soko la ajira hakuna utajiweka tayari kulitengeneza.

(Note)Katika utafiti wa soko la ajira pata taarifa sahihi kutoka kwa watu wanaohusika na soko husika na si kuuliza uliza kwa kila mtu.
     4.       SHIRIKIANA NA WATU WENYE MAENDELEO MAZURI KITAALUMA
     Shirikiana na watu ambao utanufaika kielimu kutoka kwao na wale wale wenye mwelekeo wa kile unachokitafuta.
Kwa mbinu hizi chache ninaimani zitakuongezea nguvu katika ushindani wa elimu na hivyo utakuwa sio muhitimu tu bali muhitimu bora kwa manufaa yako na kwa jamii iliyokuzunguka.





MBINU ZA KUSHIDA DHANA POTOFU ZA ELIMU

Lengo la mada hii ni kutaka kukukumbusha kuwa kuna dhana potofu zinazo husu elimu.Dhana hizo ambazo naziita potofu kwa kuwa zimekuwa hazina uhalisia wowote zaidi ya kurudisha nyuma maendeleo ya wasomi wetu.Dhana potofu ni fundisho linalodhaniwa kuwa ni kweli wakati si kweli au ni uongo unaodhaniwa kuwa kweli hivyo kuaminiwa na wengi.Miongoni mwa dhana hizo ni kama ifuatavyo:-
     1 .     ELIMU HAINA MSAADA WOWOTE  BILA PESA

kumekuwa na dhana hii kwa muda mrefu sasa.Imewafanya watu wengi hata wale walio masomoni wakati mwingine kuachana na masomo na kukimbilia kutafuta pesa ndipo warudi kutafuta elimu.

 Sina maana kuwa kama unasoma huwezi kutafuta pesa, bali natilia mkazo kuiondoa dhana hii ili wale walio katika mazingira ambayo hawawezi kufanya vyote, wajitahidi kumaliza madaraja yao ya elimu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kiutafutaji.

Dhana hii haina ukweli wowote na hutumiwa na watu wasiopenda elimu kwa kupenda njia fupi na za mkato.kupitia elimu ndipo tunapokuwa na mipango mizuri ya upataji pesa.Elimu hii kama hatukuipata darasani tutalazimika kuitafuta nje ya darasa.Endapo tutakuwa na elimu tena elimu ya kutosha kuhusiana na jambo lolote lile ,ndipo tutakapokuwa na fursa za kutosha katika kutafuta pesa.

MFANO,Mfanya biashara msomi endapo atapoteza biashara yake katika mazingira ya aina yeyote, bado atakuwa na nafasi kubwa ya kupata ufumbuzi wa tatizo lake kupitia elimu aliyonayo.Kupitia elimu aliyonayo atakuwa na nafasi ya kushindana katika soko la ajira na kupata kazi ya kufanya itakayompatia mtaji mpya.Pia ananafasi kubwa ya kuendeleza biashara yake kwa kuwa na nyenzo za kutosha kukuza biashara.Nyenzo hizo ni pamoja na-

·         Anajua kusoma na kuandika hivyo atatumia fursa hiyo kuratibu biashara yake kwa kuhifadhi
kumbukumbu,kusoma vipeperushi na majarida kwa ajili ya kupata taarifa muhimu za biashara inayomuhusu.
·         Ataadika mchanganuo wa biashara kwaajili ya kupata mikopo kwenye taasisi  za fedha  tofauti na mtu asiye na elimu ambaye atalazimika kuitafuta  elimu hiyo wakati huo.
·         Endapo biashara itakuwa kubwa bado atakuwa na fursa ya kuisimamia kwa kuwa anao ujuzi wa kusimamia biashara na kufanya shughuli za kiofisi.
kivyovyote vile kazi anazoweza kufanya mtu asiye soma mtu yeyote aliyesoma anaweza kufanya .Lakini cha kusikitisha ni kwamba sio kazi zote anazoweza kufanya mtu aliyesoma asiyesoma anaweza kufanya .Hapo unaweza kuona jinsi mtu aliye na elimu anavyokuwa na wigo mpana katika kutafuta mafanikio bila hata kuwa na pesa.



      2 .       KUFANIKIWA SIO LAZIMA UWE NA ELIMU
Ikumbukwe kuwa watu wote waliofanikiwa wametumia elimu. kama hawakuitumia rasmi basi waliitumia bila wao kufahamu.Kitu kisicho fahamika ni kuwa hawakutumia elimu rasmi katika kufanikiwa kwao kutokana na sababu mbalimbali.

*Wapo wasiotumia elimu hiyo rasmi kwa kuwa hawakuwa na uwezo wa kuifikia.
*Wapo waliokataa kwa makusudi kwa kudhani kuwa kusoma kwanza ni kupoteza muda.
*Wapo walioikosa kutokana na sababu za kukatishwa kutokana na maswala yaliyokuwa nje ya uwezo wao na sababu nyinginezo.


Kwa wale waliofanikiwa bila kupata elimu ,Kuna uwezekano mkubwa kuwa walitumia nguvu nyingi sana kuliko mafanikio waliyoyapata. Sababu  kubwa  ni kuwa walifanya vyote kwa wakati mmoja yaani kutafuta elimu huku wakitafuta mafanikio.Kwasababu hiyo kwa mtu anayetaka mafanikio yatakayoendana na kiasi cha nguvu anayowekeza ni lazima akubali kujielimisha kwanza.


      3.       UNAWEZA UKASOMA  NA USIPATE KAZI
Hii nayo ni dhana potofu .Imetumiwa na watu wengi katika kujifariji na kutochangamkia fursa za elimu kwa kuogopa kuwa watapoteza muda wao kusoma kisha wasipate kazi.Watu wenye mitazamo ya namna hii mara nyingi wamefikiri zaidi kuajiriwa kuliko kutengeneza ajira .
Mtu mwenye elimu kama ataitumia elimu yake sawasawa anaweza kutengeneza ajira yake binafsi na baadaye kupitia ajira yake akazalisha na za wengine.

mfano muhitimu wa daraja la diploma wa chuo cha hoteli badala ya kuzunguka mwaka mzima akitafuta kazi ya umeneja mahotelini na kuambulia mshahara kiduchu.Anaweza kutumia elimu aliyoipata kufungua mgahawa wake mitaa ya nyumbani kwake na kutengeneza vyakula asili vya watu waliomzunguka .kwa kutumia ujuzi mkubwa alionao ni wazi kuwa huduma zake zitakuwa bora kuliko wale wote wanaofanya shughuli hizo bila elimu, hivyo kuvuta wateja wote kwake.Ni dhahili kuwa baada ya miaka michache asizungumze tena kuhusu kuandaa vyakula bali kumiliki mgahawa wa kisasa kama si hoteli.

Pia hata kwa wahitimu wengine wanaweza kuanzisha ajira zao wenyewe kupitia wao binafsi au vikundi kulingana na taaluma husika. Hivyo si kweli kwamba kuna mtu anaweza akasoma na asipate cha kufanya.



      4.       UKISOMA SANA HUTAPATA AJIRA KWA KUWA WAAJIRI WATAOGOPA KUKUAJIRI
Dhana hii nayo siyo sahii japo hata baadhi ya wasomi wamekuwa wakiitumia.Kinachotakiwa ni kufikiri zaidi jinsi utakavyoitumia elimu kubwa utakayokuwa nayo na si jinsi watu wengine watakavyoitumia elimu kubwa uliyonayo.

Uwoga huu ndiyo unaoleta dhana hizi potofu na kuzifanya ziwe na nguvu katika jamii.Elimu ya kiwango cha juu ndiyo inayohitajika katika dunia.Mtu mwenye kiwango kikubwa cha elimu si bidhaa tu kwake na kwa  kwa wanaomzunguka bali ni bidhaa pia katika ulimwengu .Elimu kubwa inahitajika kwa mtu binafsi,kwa jamii inayomzunguka na hata kwa ulimwengu mzima.

Sote ni mashahidi wa mageuzi makubwa yanayofanyika ulimwenguni.Iwe ni mageuzi ya kiteknolojia ,kiuchumi,kielimu,kitabibu,nk mengi yamefanywa na watu waliobobea katika elimu husika.

Sina maana kuwa watu wasio na elimu kubwa hawana mchango katika maendeleo,bali walio na elimu ya kati wakisaidiwa na wenye kiwango cha juu cha elimu ukijumlisha na vipaji walivyonavyo wanafanya maajabu zaidi.

fikiri kuwa elimu vyuoni ingekuwaje kama kusinge kuwa na watu waliobobea kufundisha,mahospitalini matibabu yangekuwaje kama kusingekuwa na mabingwa,katika biashara na uchumi, sote ni mashahidi juu ya mitikisiko ya uchumi duniani kuwa  tulihitaji watu waliobobea kiuchumi.
Bila shaka iwe ni kwa matumizi binafsi au ya umma, kusoma sana ni muhimu kwaajili ya maendeleo.

      5.       WASOMI WA ZAMANI NDIYO BORA KULIKO WA SASA
Kuna wanaodai kuwa wasomi wa zamani ni bora kuliko wasomi wa sasa hivyo kisomo cha sasa hakina tija.Dhana hii imezungumzwa hata na baadhi ya watu wanaoheshimika katika jamii.Kwa kiasi kikubwa umma umepotoshwa na dhana hizi potofu kiasi cha kutowapa umuhimu wasomi wetu wa sasa kwa kigezo kuwa hawana lolote.

Wasomi ninaowazungumzia hapa ni wa aina zote wawe wale wa kiwango cha shule za msingi au chuo kikuu.Kwa mujibu wa dhana hii wameonekana kuwa hawana lolote na kwa sababu hiyo wale wahitimu wa zamani ndiyo walio bora.Na wengine hasa hapa kwetu tz wamedai kuwa mwanafunzi wa darasa la saba wa mwaka 76 ni bora kuliko Yule wa kidato cha nne cha sasa katika miaka hii ya 2000.

Kunakitu ambacho tunakisahau na ndiyo maana dhana hii inapata nguvu kiasi.Tunachotakiwa kufahamu wakati  tunapofanya malinganisho ya wahitimu hawa tunatakiwa kuangalia vigezo vifuatavyo.
1.       Umri wa wahitimu wa sasa na wale wa miaka ya nyuma
2.       Mitaala ya sasa na ile ya zamani
3.       Fursa za sasa na zile za miaka ya nyuma

UMRI
tukianza na hilo la umri ni wazi kuwa wahitimu wengi wa sasa kwa ngazi yeyote ile wanaumri mdogo kuliko ule wa wale wa miaka ya nyuma.Mfano miaka ya nyuma kwa hapa kwetu Tanzania mwanafunzi wa darasa la saba alikuwa na umri mkubwa kiasi cha kufikia hata 20.Lakini kwa wanafunzi wa sasa wengi wao wana umri wa miaka 14 na 15.

kwasababu hiyo wanafunzi wa sasa wanauwezo mkubwa kifikra kuliko wale wa miaka ya nyuma .Kwasababu mtoto wa sasa wa miaka13 na 14 anauwezo wa kujifunza na kushika mambo ambayo wakati huo yalikuwa yakisomwa na mwanafunzi wa miaka 18 na 20.
Lisha ya hapo wanafunzi wa sasa waanajifunza mambo mengi na Wakihitimu Wanatija kubwa  kuliko wale wa miaka ya nyuma .Ukichukua mwanafunzi wa kidato cha nne wa miaka ya sasa ambaye wastani wa umri wake ni sawa na Yule wa darasa la saba wa miaka ya nyuma yaani miaka 18  mara anapohitimu ,kulingana na mtaala uliopo anafahamu mambo yafuatayo

1. Anafahamu kuhusu mambo yote yanayohusu mwili wake ikiwamo mifumo yote muhimu ikwamo ya uzazi na jinsi ya kujikinga na baadhi ya magojwa.
2.Anafahamu kwa sehemu kubwa mgawanyiko wa wanyama na tabia zao pamoja na mimea na makundi yake na sifa zake.
3 . Anafahamu kuandika barua mbalimbali za kiofisi ikiwamo za kuomba kazi na kuandaa ripoti.
4.Anafahamu kemikali mbalimbali zenye manufaa na zile zisizo na manufaa
5.Anafahamu uandishi wa insha na muhutasari wa maswala mbali mabali ya kijamii.
6. Anafahamu kwa sehemu kubwa utunzaji wa kumbukumbu
7.Anafahamu kwa sehemu kubwa nguvu za asili zilizopo duniani na jinsi zinavyoweza kupimwa.
8. Anafahamu tabia nchi na mambo yote yanayohusiana na tabia nchi ikiwamo hali ya hewa na vipimo vinavyotumika kipimia.
9.Anafahamu historia ya nchi yake na Afrika, madhara ya ukoloni na faida zake,madhara ya kutokuwa na umoja nk.
10.Unafahamu maswala muhimu ya uraia pamoja na haki na wajibu wa raia.
11.Anafahamu mifumo kadhaa ya kisasa ya mashine na jinsi inavyofanya kazi.
12.Anaelimu ya mauzo na manunuzi
13.Anafahamu matumizi ya komputa na faida zake
14.kama ni mwanafunzi wa shule za ufundi ana jua uselemala,ujenzi,upauaji,na mambo mengine ya ufundi.


Muhitimu huyu kama nitaamua kuandika habari zake zote ni wazi kuwa ukurasa huu hautatosha.kwa ushahidi huu naweza kusema kuwa muhitimu huyu wa sasa anatija kubwa kwa kuwa katika umri mdogo tayari anafahamu vitu vingi.

Mifano ya ushahidi wa manufaa hayo ni wamefanya vizuri katika majeshi yote,viwandani,katika biashara ndogo na kati,katika kilimo nk.
MTAALA
Mtaala wa zamani ulilenga kumwandaa mwanafunzi kuishi katika ujamaa na kutumia rasilimali zilizomzunguka.Lakini mtaala wa sasa unalenga kumwandaa mwanafunzi  kuendelea na elimu inayofuata vilevile kuingia katika soko la ajira.Mpaka hapa utaona jinsi mwanafunzi wa sasa alivyo na tija zaidi.

FURSA.
Hili ndilo swala linalosababisha wahitimu wa sasa waonekane hawana lolote .Wahitimu hao ni pamoja nawale wa vyuo vikuu.Wahitimu wa sasa wanachokikosa ni fursa.Wengi wao wanaonekana hawana lolote kwasababu ya kukosa cha kufanya.Wakati wa miaka ya nyuma wahitimu wote waliingizwa kazini kinyume na wahitimu wa sasa ambao baada ya kumaliza masomo yao wamejikuta wakigonga ukuta katika soko la ajira.Takwimu zilitolewa hivi karibuni na BARAZA LA VYUO VIKUU AFRIKA MASHARIKI  zinaonyesha kuwa  nchini Tanzania ni 38% tu ya wahitimu wa vyuo ndiyo wanaopata ajira baada ya kuhitimu masomo yao.

 Aidha kwa mujibu wa takwimu za wizara ya kazi na ajira za mwaka 2006 kupitia utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi ulibaini kuwa,jumla ya wahitimu wa stashahada 1.160 kati ya wahitimu 35,875 hawakuwa na ajira na jumla ya wahitimu 3,092 kati ya 45,600 wa shahada na stashahada za juu hawakuwa na ajira nchini Tanzania.

kwasababu hiyo kilichopo ni kuwaimarisha wahitimu waweze kujiamini na kutengeneza ajira binafsi.







       6.       ELIMU NI GHARAMA SANA HIVYO WENYE PESA NDIYO WANAOMUDU
Kifupi naweza kusema kuwa elimu ni gharama kama utahitaji elimu ya namna hiyo.Kwa mtu anayehitaji elimu kwa gharama ndogo anaweza kuipata.Kwa mtafuta elimu atatumia njia zote za kutafuta elimu ikiwamo maktaba ambazo zimekuwa zikitoa fursa ya watu kupata elimu kwa gharama inayoweza kumfanya kila mtu kumudu.

      7.       SIO VIZURI KUSOMA VITU VINGI
kifupi naweza kusema kuwa hakuna utafiti wowote wa kisayansi uliopendekeza kuwa kusoma vitu vingi kunamadhara .Utafiti umeonyesha kuwa ubongo wa mwanadamu unauwezo wa kuhifadhi kumbukumbu zote tangu kuumbwa kwa mwanadamu hata dunia itakapoisha  na bado kukawa na nafasi katika ubongo.Utafiti uliofanywa umeonyesha kuwa ubongo unahifadhi kumbukumbu taratibu sana ,Hivyo hakuna hofu kuwa ukijifunza vitu vingi eti sio sawa.

kulingana na mchango huu hata kama hautakidhi kikamilifu kukuondoa kwenye dhana potofu zinazohusu elimu bali utakuwa umenufaika katika maeneo machache niliyoyagusia japo nimefanya hivyo kwa kifupi.



Jumatano, 21 Mei 2014

JINSI YA KUFAULISHA MITIHANI KIDATO CHA NNE TANZANIA



Hivi sasa Tanzania kumekuwa na mfurulizo wa kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa kasi kubwa.Shwala hili limeleta mvutano na malalamiko mengi miongoni mwa jamii hususani wapenda elimu.

Malalamiko yaliyojitokeza kufuatia kushuka kwa kiwango cha ufaulu ni kama ifuatavyo:-

1.Serikali imeshindwa kuboresha mazingira ya elimu yaani hakuna ,shule za kutosha,vitabu,maabara,walimu,waliopo wengi wao wamepata mafunzo ya muda mfupi,kiwango cha ufaulu cha wanao kwenda kusoma ualimu ni cha chini mno, mishahara midogo,kutelekezwa kwa shule za kata, mengine ni:-

masomo ni mengi kupita uwezo wa uelewa wa wanafunzi,matumizi ya lugha ya kigeni kufundishia,mfumo mbovu wa elimu yaani kubadilika badilika kwa mtaala, nk.

2.Walimu wamelalamikiwa kwa kujali zaidi shughuli binafsi kama tuition na kadhalika kuliko kufundisha darasani.

3. Wasimamizi wa elimu hawaja chukua majukumu yao ya msingi kusimamia elimu ipasavyo, nk.

4.ukosefu wa nyumba za walimu na mabweni kwa wanafunzi wa kike.

Pia kumekuwa na malalamiko mengine mengi ambayo serikali inalaumiwa ambayo nisingeweza kuyataja kutokana na uwingi wake.

MASWALI YA KUJIULIZA KABLA YA KULAUMU

1.Kama kiwango cha elimu kimeshuka kutokana na upungufu wa shule je ni lini huko nyuma shule zilitosha na kutapakaa kila mtaa na ndiyo ikawa sababu ya ufaulu mkubwa?.

2.Ni lini siku za nyuma vitabu,maabara,na vifaa vingine vya kufundishia vilitosha na ndiyo maana tulikuwa na ufaulu mkubwa?

3.Ni lini waalimu walitosha siku za nyuma ndiyo maana tulikuwa na ufaulu mkubwa?

4.Ni wakati gani siku za nyuma serikali ilikuwa ikipeleka wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza kusomea ualimu na ndiyo sababu tukawa na ufaulu mkubwa?

5.Kuhusu mafunzo ya muda mrefu je! Hatukuwahi kuwa na walimu wa UPE na wakafanya vizuri siku za nyuma?

6.Kuhusu kubadilika kwa mitaala, je ! kuna umuhimu wowote kuendelea kubaki na vitu ambavyo vimekwishapitwa na wakati katika mitaala ili kuzalisha division one?

7.Kuhusu matumizi ya lugha ya kigeni ,je! kunawakati tuliwahi kutumia Kiswahili kufundishia siku za nyuma? Katika somo la Kiswahili utafiti umeonyesha kuwa watoto wote hupata daraja la kwanza?

8.Kuhusu mishahara ,inamaana wale walimu wa zamani walikuwa wakilipwa kwa masaa kama ilivyo kwa baadhi ya maprofesa wanaofundisha vyuo zaidi ya kimoja?

Ni wazi kuwa kila swali jibu lake ni HAPANA. Hiyo inaonyesha kuwa kuna kitu tunacho kisahau wakati wa kufanya majumuisho nani wa kumlaumu na nini tufanye kuokoa ufaulu wa watoto wetu.

NINI CHA KUFANYA KUONGEZA UFAULU


Tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu sababu za kushuka kiwango cha ufaulu zililenga taasisi za elimu. Tafiti hizi ni pamoja na zile za serikali yenyewe na hata za taasisi za kiraia kama TWAWEZA nk.Vile vile tafiti hizo nyingi mapendekezo yake yahusisha gharama kwa serikali.

Lakini swala la kuanguka kwa ufaulu ni zaidi ya taasisi za serikali. Kuna uwezekano wa kuleta mabadiliko bila ya kutumia gharama kubwa kama tunavyodhani .Hili tumeliona kupitia mitazamo ya watu wengi hata kwa baadhi ya viongozi wa serikali kama wabunge na wengineo.Wengi wamekuwa wakilalamikia bajeti ndogo ya elimu inafanya kiwango cha ufaulu kushuka bila kujua kuwa huko nyuma tulikuwa na bajeti ndogo kuliko hizi za sasa.

katika swala hili kila mtu anachangia kwa namna yake ikiwamo mimi na wewe.Na kama kweli tukiamua kukomesha tatizo hili tuna uwezo wa kubadili matokeo ndani ya mwaka mmoja.Ila kama tutaendelea kumtafuta mchawi basi mpaka masihi atakaporudi bado atakuta tuna mtafuta mchawi na hatutampata.

Kuna hatua za ujumla za kuchukua ili kunusuru janga hili na wala hazihitaji gharama ya ziada nazo ni kama ifuatavyo:-

1.KUDHIBITI VYETI FEKI


Hili ni swala linalomuhusu kila mtu.vyeti feki ni vile vyeti vinavyotumiwa na baadhi ya walimu wanafunzi katika kujipatia fursa ya kusoma ualimu bila kuwa na sifa halali.Hawa ni watu wenye shida ya ajira lakini hawana lengo la kufundisha watoto.Wamekuwapo shuleni kutimiza idadi lakini mchango wao hauna tija hata kidogo.mimi na wewe tukikataa kuwapa vyeti vyetu au kuwatengenezea vyeti feki basi hakutakuwa na walimu wa namna hii.
Serikali kwa upande wake iwa badilishe wale walioingia kwa vyeti feki kwa kuwaweka wale halali.

2.WALIMU WALIOPO WAFUNDISHE.

Bila kujali uchache wao au kuchelewa kwa posho walimu waliopo wafundishe.Hata kama shule inamwalimu mmoja anatakiwa afundishe.kwa kufanya hivyo atakuwa ametimiza jukumu lake la msingi. Wale wanafunzi waliopata nafasi ya kuhudhuria shule siku hiyo watakuwa wamejifunza.Wanafunzi wanachokitaka sio uwingi wa walimu bali ni ubora na uwingi wa topic.


Kitendo cha walimu wa sasa kutumia kisingizio cha kuchelewa kwa posho ,malipo ya uhamisho nk.kutofundisha hakina mashiko.Hapo awali kulikuwa na usumbufu zaidi ya huo lakini bado ufaulu ulikuwa unaridhisha.Walimu wote walikuwa wakilipwa fedha zao mkononi na wengine walikuwa wakifuata mshahara zaidi ya kilometa mia tano safari ya masaa nane kwa basi.Lakini katika kipindi hicho chote bado kulikuwa na ufaulu unaoridhisha.vipi kuhusu hawa wa kidigitali wakibofya tu wanazoa ufaulu kwa nini hauvunji chati?

3.VITABU VILIVYOPO VITUMIKE

Kumekuwa na kawaida ya kufungia vitabu stoo kwa baadhi ya shule na kuwaacha wanafunzi wakiwa wanasoma bila kitabu kwa lengo la kuvihifadhi.Tunachotakiwa kufanya ni kuwapatia wanafunzi vitabu vilivyopo na kuwasimamia kuhakikisha kuwa wanavitumia kwa manufaa.Siku za nyuma kitabu kimoja kilitumika hata kwa watoto sita na ufaulu bado ulikuwa juu.


Wapo waliosoma mpaka wanamaliza hawakuwahi kuona baadhi ya vitabu na walifaulu.Kinachotakiwa sio utitiri wa vitabu bali ni vilivyopo vinatumikaje.


4.TUTUMIE MAABARA ZILIZOPO

Ili mwanafunzi aweze kuelewa sio lazima alale maabara.Anahitaji majaribio machache tu kulingana na topic anayosoma.Na wala sio majaribio yote yanahitaji maabara, mfano kujua mfumo wa uzazi wa panya sio lazima jaribio lifanyikie maabara, bali vifaa vichache tu vinavyoweza kuandaliwa hata na mwanafunzi mmoja tu na jaribio likafanyika.

Pia tunaweza kutumia mfumo shirikishi wa maabara.ZOEZI hili ni rahisi sana hasa kwa shule za umma.Shule zinaweza kuanzisha mfumo wa kushirikiana katika kutumia maabara moja wakati wakisubiri zakwao kujengwa.

Maabara moja inaweza kutumiwa na shule hata tano kwa kwa mfumo wa matumizi shirikishi.Kama shule zimeweza kushirikiana katika mashindano ya shule za sekondari ,NA majaribio ya mitihani mbalimbali kwanini zisiweze kwa mambo ya msingi kama haya ya maabara?.

5.TUACHE KUELEKEZA MACHO KUJENGA MASHULE TUU.

Huu upepo wa wazazi kuelekeza macho kwenye kujenga mashule bila kushiriki katika swala la ufaulu linachangia kushusha ufaulu.

Nguvu hii tuliyoitumia katika kujenga mashule tuitumie katika kuinua kiwango cha ufaulu.Wanajamii tunaweza kuanzisha na kudhamini MASHINDANO ya TAALUMA ya KIKANDA kwa SHULE za SEKONDARI ya kila baada ya miezi sita ambapo watoto hamsini wa kwanza wanazawadiwa vifaa muhimu vya shule.ambayo tunaweza kuyaita( MATAKISHUSE).


Hapa tunakuwa tumepiga ndege wawili kwa jiwe moja ,kwanza tutakuwa tumewapa watoto mwamko wa kufanya vizuri ili washinde,tutakuwa tumewawezesha kupata mahitaji muhimu ya shule,wazazi watasimamia watoto wao ili washinde ili wanufaike na zawadi.Na hili linawezekana kama ilivyowezekana kudhamini michezo ya wazee wazima ya kila mwaka kama ya mashindano ya michezo ya vyombo vya habari nk.

Wazazi baada ya kujenga mashule mengi sasa imefika wakati wa kuamua watoto wetu wasome kwa raha bila karaha.

Mfano Badala ya kuendelea kuchangia kila siku swala moja la madawati na matokeo yake dawati moja linakwenda kununuliwa na wajanja wachache hata kwa shilingi milioni moja, sasa tuchangie dawati na si fedha.Kama inakuwa ngumu kwa mzazi mmoja kuchangia dawati moja basi wazazi wawili wanaweza kuchangia dawati moja.Na hili linawezekana kwa kuwa rasilimali zote za kutengenezea madawati tunazo ikiwamo mafundi.

6.TUREJESHE MAADILI

Kama kuna kitu ambacho kimefanikiwa kuua elimu kwa kiasi kikubwa basi maadili naweza kuyapa nafasi ya kwanza.Hakuna mtu anaye hitaji kufundishwa maadili na hakuna mtu anayeweza kusomea maadili na akafuzu. Maadili ni tabia na tabia hufundishwa kwa kuambukizwa na anayeambukiza tabia lazima awe nayo.

Tuwaambukize watoto maadili mema.Hili ni kwa kila mtu kuanzia mzazi,mpitanjia hata kwa mwalimu.Kama mwanafunzi akiwa na maadili akiambiwa sikiliza atasikiliza,akiambiwa andika ataandika,akiambiwa kesho mapema atafika mapema nk.

Tuache kuwaalika wanafunzi katika kumbi za starehe,tusishirikiane nao tunapowaona katika mazingira kama hayo,tuwaelekeze kuheshimu wakubwa kwa kuanza kuwaheshimu wao,tufuatilie mahudhurio yao hata kama hawatuhusu kwasababu hao ndio Tanzania yenyewe.Wakifanya vibaya tunadhalilika wote.

7.WAZAZI WAWAJIBIKE

Wazazi wasiachie shule kila kitu.Mtu wa kwanza kutoa elimu kwa mtoto ni mzazi.Mzazi anafundisha kula,kuvaa,kusalimia,usafi,nk.Lakini linapofika swala la kusoma na kuandika anajitoa, hii si sawa.

Mzazi anawajibu zaidi ya mwalimu kuhakikisha kuwa mtoto anajua kusoma na kuandika na hata kufikia kikomo cha upeo wa mzazi husika.

Maendeleo ya uelewa wa mtoto yanaweza kupimwa zaidi na mzazi kwa kuwa yeye ndiye anayejua hata sababu ndogondogo zinazomfanya mtoto kutokufanya vizuri shuleni.

8.TUWASAIDIE WANAFUNZI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA ELIMU

Wanafunzi wa sasa wanakabiliana na changamoto nyingi sana tofauti na wale wa zamani.
KUTOKANA NA MAENDELEO YA KIUCHUMI watoto wa sasa wanapendeza kimuonekano na kusababisha mizee mizima kuwamezea mate.kwa sababu hiyo wanarubuniwa na kutumia nguvu nyingi kuzingatia masomo.Tuingilie kati mara tunapoona wanapotoshwa na kushawishiwa kukiuka miiko ya wanafunzi.

9.TUWAFUNDISHE KUTUMIA TEKNOLOGIA KIMANUFAA

Siosawa kuwazuia watoto hawa kutumia simu wala computer wakati ndivyo vifaa vinavyotumika katika zama zao kurahisisha shughuli za kila siku.
Chakusikitisha ni kwamba wakati unawazuia wao wanatumia kwa siri.Matokeo yake wanatumia isivyosahihi kwa kuwa hawajui kuwa kunauwezekano wa kunufaika na vifaa hivyo vya teknologia ya sasa.

Kitu cha msingi tuwafundishe wanafunzi wetu matumizi sahihi ya teknologia hizi za sasa na namna wanavyoweza kunufaika nazo kwa kuongeza ufaulu wao.

MATUMIZI YA INTERNET

Mfano ,kupitia simu au laptop mwanafunzi anaweza kudownload notes kwenye mtandao au kutoka kwenye faili la kimtandao la mwalimu wake na kujisomea au kushare na wanafunzi wenzake. Atajuaje haya kama hakufundishwa?

Wanafunzi wanaweza kuanzisha blog yao , website au group lao katika mitandao ya kijamii na kushirikiana katika mijadala ya elimu na kubadilishana notes pamoja na mswali kwa mazoezi.Je wasipoelekezwa kutumia fursa hizi watajuaje?

Kama wanafunzi wakielimishwa zaidi wanaweza kutumia simu zao hata darasani kwa usimamizi maalumu kujifunza baadhi ya vitu ambavyo sio rahisi kupatikana katika mazingira yao.kupitia mtandao wa internet vitu ambavyo wanafunzi wanaweza kujifunza ni pamoja na,

1. Uhalisia wa sasa wa sayari wanayoishi katika picha za hivi karibuni bila kusubiri vitabu vibadilishwe.

2. Mabadiliko mapya ya kisayansi ambayo bado hayajaingizwa kwenye vitabu

3. Mazingira halisi ya maeneo ambayo wamejifunza bila kufika kwa kutazama video zake katika mtandao au simulizi za picha zake.

4. Shughuli mbalimbali za kiutafiti,takwimu,hotuba za viongozi ,historia za nchi mbali mbali nk.

5. Ufafanuzi wa ziada wa baadhi ya topic ambao haumo kwenye vitabu.

6. Taarifa zinazobadilika badilika kama za viongozi wakuu wa nchi na taasisi zake zinazowekwa katika mtandao na mengine mengi.

7. kutumi website zilizo na baadhi ya notes wanazozihitaji kujisomea na kuongeza ufaulu.

8. Kutumia kamusi za kimtandao kupata ufafanuzi wa maswala ambayo hayapo kwanye kamusi zilizo chapishwa au vitabuni.

10.MWANAFUNZI AFANYE WAJIBU WAKE

Wajibu mkubwa wa mwanafunzi ni kusoma na si vinginevyo.kama elimu yake inapatikana shuleni basi apatikane shuleni na asionekane maeneo mengine baada ya muda wa shule.mwanafunzi awe na uchaguzi wa mambo ya kushirika na si kila jambo.


Japo kuna mambo mengine ambayo mwanafunzi anaweza kufanya huku akisoma lakini si yote yanaurafiki na elimu.Ni wajibu wa mwanafunzi kuchagua masuala ya ziada ya kufanya yenye urafiki na elimu wakati wote wa masomo yake.

Wakati akitafuta mambo yanayokubaliana na elimu anatakiwa ajiepushe kabisa na yale yanayo mfanya ashindwe darasani.

Mwanafunzi hazuiliwi kujiburudisha lakini inategemea sana na burudani anayoitumia kama inaurafiki na elimu.

MAPUMZIKO SALAMA

Mfano mwanafunzi badala ya kwenda beach na kukaa bure anaweza kufunga safari na kwenda sehemu za makumbusho na kufanya mapumziko yake hapo.Kwa kufanya hivyo anakuwa amepumzika pia ameongeza uelewa wa mambo ya kale.

Kwa wale wanaoishi karibu na hifadhi za kitalii wanaweza kutumiafursa hiyo kutembelea hifadhi hizo kwa gharama ambayo kila mmoja anamudu.

Wakati wa mapumziko marefu mwanafunzi anaweza kujiunga na shughuli mbali mbali za kiuzalishaji kwa ajili ya kujijengea uwezo wa kiuzalishaji baada ya kumaliza masomo .

Mfano mwanafunzi anaweza kujiunga kimafunzo katika shughuli ya ufugaji kuku wa kisasa,uchongaji wa vinyago,uchoraji,ushonaji,uhunzi,mapishi,kuendesha biashara za duka,genge,shughuli za stationary , huduma za internet nk.

Vilevile mwanafunzi anaweza kutumia muda wake wa likizo kutembelea shughuli za kiviwanda,kielimu kama vyuo mbalimbali,mahakama kusikiliza kesi,hospitalini kujionea wagonjwa na huduma zinazotolewa,kutembelea vituo vya watoto yatima,mashamba makubwa na madogo kujionea kilimo kinavyoendeshwa nk. katika maeneo yote hayo mwanafunzi anakuwa amepata uzoefu wa mambo mbalimbali kulingana na eneo husika.
Kwa kufuata mazingira yanayomjenga mwanafunzi siku zote atabaki salama na ufaulu wake kuongezeka siku baada ya siku.

Ni imani yangu kuwa kama tutazingatia hayo kiwango cha ufaulu kinaweza kuongezeka na kuzidi kile cha siku za nyuma hata bila kutumia gharama kubwa za kifedha kama wengine ambavyo tumekuwa tukifikiri.