CURRICULUM

JINSI TUNAVYOWEZA KUTUMIA MITAALA TZ KUINUA VIPAJI.
Kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu mitaala ya Tanzania kwamba haikidhi matarajio ya mwanafunzi kwa maisha yake baada ya kutoka shule.
Mfano;-
wakilalamikia
1.watu wengi wamekuwa kuwa mitaala iliyopo haimuandai mototo kuishi maisha ya kujitegemea baada ya kumaliza masomo yake.Wangependa mwanafunzi akimaliza sekondari awe mjasiriamali,mkulima nk.

2. Malalamiko mengine ni kuwa watoto wamekuwa wakisoma masomo mengi kupita kiasi ,Kitu kinachomfanya mwanafunzi kuwa na mzigo mkubwa wa mambo ya kujifunza.Wangependa kuona wanafunzi wanasoma masomo machache tu ili wayamudu.

3. Pia wamekuwepo watu wanaodai kuwa mambo ambayo wanafunzi Tanzania wanajifunza hayahusiani na maisha tunayoishi.Yaani wanajifunza mambo ambayo hatuyahitaji katika maisha yetu.

4. Wapo wanaodai kuwa eti elimu inayotolewa Tanzania bado ni ya kikoloni na siyo ya kiuzalishaji kama inavyokusudiwa.
5.Wapo wanaodai kuwa elimu ya ujasiriamali haijapewa kipaumbele katika elimu ya Tanzania.

6.Maswala ya kijamii nayo yamelalamikiwa kuwa eti hayajawekewa mkazo katika elimu ya tazania.Inamaanisha kuwa eti inawafanya watu wasiwe wanajua haki zao, wasiwe wawajibikaji,waadilifu,nk.

7.Michezo vivyohivyo imelalamikiwa kuwa haijatiliwa mkazo katika elimu ya Tanzania.Kwamba watoto hawajafundishwa michezo kama somo rasmi nk.

8.Hata maswala ya kilimo yamezungumzwa kutozingatiwa katika elimu ya Tanzania.Baadhi ya malalamiko yanadai kuwa wahitimu wengi hawapendi kufanya kilimo kwakuwa hawakufundishwa kilimo mashuleni.

Nitakubaliana na malalamiko hayo kwa sehemu ndogo sana .Lakini cha kushangaza ni kwamba malalamiko mengi yanatokana na kutoifahamu mitaala yenyewe.Cha ajabu zaidi ni kwamba hata watu wenye elimu wamekuwa wakiilalamikia mitaala kwamba ndiyo kikwazo cha maendeleo ya Tanzania.Kifupi ni kwamba malalamiko mengi sio ya kweli na hayatujengi,hivyo yanatunyima fursa ya kutumia mitaala iliyopo kikamilifu ili kuleta tija kwa taifa letu.

Kwa kuupitia mtaala wenyewe kwa ufupi ninaimani sote kama wadau muhimu wa elimu yetu Tanzania, tutagundua mambo mazuri na hatimaye kuyatumia kama mtaji, katika kuibua na kuboresha vipaji vya wanafunzi wetu.

(I) MAANA YA MTAALA
Wataalamu wa masuala haya wanadai kuwa mtaala una maana nyingi sana kutokana na dhana tofautitofauti . Taarifa ya TAASISI YA ELIMU YA MWAKA 2013 MARCH ya maboresho ya mitaala tangu mwaka 1961 hadi 2010,inadai kwamba dhana ya mtaala, ikijumuisha nadharia zake na muundo wake (models) ni eneo la taaluma lenye mitazamo (perspectives) tofauti.

Lakini taarifa ya taasisi hiyohiyo na mwaka 2005 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2013 ya mtaala wa elimu ya secondary iliyoandikwa kwa lugha ya kiingereza katika utangulizi wake inasema ( Curriculum is generally prescribed as a set of standards that guides the delivery of education by considering the following areas:) mtaala ni viwango vilivyopangwa au kuwekwa na serikari ili kuongoza utoaji wa elimu kwa kuzingatia maeneo yafuatayo;-

Maeneo hayo ndiyo yale yanayotajwa na taarifa ya mabadiliko ya mitaala tangu mwaka 1961-2010, iliyotolewa mwezi march 2013 nayo ni –

(i) Ujuzi watakaoujenga wanafunzi (competences) yaani maarifa (knowledge), stadi (skills) na mwelekeo (attitudes),
(ii) Njia za kufundishia na kujifunzia zitakazotumika katika utekelezaji wa mtaala (pedagogical orientations),
(iii) Vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinavyohitajika,
(iv) Upimaji, ufuatiliaji na tathmini ya mtaala husika.
(v) Sifa za kitaaluma na kitaalamu za mwalimu atakayeuwezesha mtaala husika,
(vi) Miundombinu wezeshi (enabling infrastructure) kwa utekelezaji wa mtaala wenye ufanisi,
(vii) Muda utakaotumika katika ufundishaji/utekelezaji mtaala

Ili kupata uelewa mzuri kuhusu mtaala hatuna budi kugusia pia na sera ya elimu ambayo ndiyo inayozaa mtaala.

TAMKO LA SERA YA ELIMU
Mtaala wa elimu ya sekondari nchini unatokana na kitu kinachoitwa TAMKO LA SERA YA ELIMU (EDUCATIONAL POLICY STATEMENT)

Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa tamko la sera ya elimu ni kwamba utoaji wa elimu katika nchi ni lazima uendane na matakwa au mahitaji ya nchi husika,na vilevile mahitaji au matakwa ya dunia.Mtaala umezingatia pia mazingira ya kijamii na ya kiuchumi bila kuacha upande wa pili yaani yatakayoendana na hali kama hizo kidunia.

Chukulia kuwa kama kila nchi ingeamua kufundisha watoto wa nchi husika kwa kuzingatia mahitaji ya nchi yao tu, leo dunia ingekuwa na hali gani,kiuchumi,kijamii,kisiasa,kidiplomasia ,nk ?.Lakini kwa kuzingatia matakwa ya dunia ya leo mtaalamu yeyote anaweza kuwa msaada au kufanya kazi popote kutokana na maandalizi aliyoyapata akiwa shuleni.

Swala hili linatupa ushahidi tosha kabisa kuwa kuna umuhimu wa kutazama na upande wa pili katika maswala haya ya elimu.Tusije tukatengeneza kizazi kitakachoshindwa kuendana na dunia kwa kukosa maarifa na ujuzi utakaokifanya kiwe nyuma au kutofiti kabisa katika dunia yaleo.Haya yote yanawezekana tu pale tutakapoachana na fikra za kuzalisha wachuuzi wa kwenda china na dubai kwaajili ya maisha ya tumbo na mavazi.

Matamanio ya watu wengi ni kuzalisha wachuuzi tu na sio wataalamu.Kama unandoto za kuzalisha wachuuzi basi mtaala huu hautakufaa kabisa kwa kuwa umelenga kuzalisha wataalamu .Mwanafunzi wa sekondari lazima ajengwe katika msingi imara wa nadharia ya mambo mengi ili achague machache atakayoyafanyia kazi mbele ya safari katika maisha yake.

Ni lazima mwanafunzi atengenezwe ili kujisaidia yeye mwenyewe ,jamii inayomzunguka na kuwa na mchango katika dunia.Kumbuka kufeli na kubaki nyumbani ni bahati mbaya tu.
Kama utausoma vizuri mtaala wa sekondari utagundua unaandaliwa kwa lengo la kumfanya mwanafunzi kuwa tayari kuendelea na masomo ya juu, na endapo hataendelea basi atatumia ujuzi huo mdogo kujikimu yeye mwenyewe kufuatana na juhudi alizonazo.

Tukumbuke kuwa kama tutaamua kuwavuna na kuwatumia kwa matumizi yetu basi bado watahitaji ujuzi wa ziada ili waweze kufaa kwa shughuli za kijamii.Mifano mizuri tumeiona kwa JESHI LA POLISI,JESHI LA WANANCHI, NA JESHI LA KUJENGA TAIFA,NA BAADHI YA VIWANDA NA TAASISI.Hawa huwachukuwa vijana hawa na kuwapa mafunzo maalumu na kuwatumia kwa kazi mbalimbali na ufanisi wake sote tumeushuhudia.Asilimia kubwa ya wazalishaji wa nchi hii ni vijana waliotoka katika kundi hili.

Sasa ili kujiridhisha kuwa mtaala unazingatia mambo yote muhimu tunayoyakusudia tutazame muhutasari wa malengo ya mtaala kwa ujumla wake kabla ya kuzama ndani zaidi .
MALENGO YA MTAALA WA ELIMU YA SEKONDARI TANZANIA
Mambo haya yameainishwa katika mtaala wa elimu kama ulivyoboreshwa mwaka 2013 nayo ni ;-

1.Kuimarisha na kupanua mtazamo wa mawazo ya msingi ,maarifa , ujuzi, na kanuni zilizopatikana na kuendelezwa shule za msingi.

2.Kuboresha maendeleo zaidi na kutambua umoja wa kitaifa,utambulisho,maadili,uwezo binafsi,kuheshimu na utayari wa kufanya kazi,kutambua haki za binadamu,utamaduni,utashi ,desturi,mila, majukumu ya kiraia na wajibu.

3.Kuinua maendeleo ya uwezo katika lugha na matumizi ya ufanisi ya ujuzi wa mawasiliano katika lugha ya Kiswahili na angalau moja ya lugha ya kigeni.
4.Kutoa fursa kwa mahitaji ya maarifa, ujuzi , jitihada, na uelewa katika eneo la kujifunza lilichaguliwa.

5.kumuandaa mwanafunzi kwa elimu ya ngazi ya tatu na ya juu,ya ufundi, ufundi sanifu,na mafunzo ya kitaalamu.

6.Kuamsha hisia na uwezo wa usomaji binafsi,kujiamini na kujiendeleza katika waanzilishi wapya wa sayansi na teknolojia,taaluma,ujuzi wa kikazi,na mbinu

7.Kuwaandaa wanafunzi kuingia katika dunia ya kiutendaji.

Nimelazimika kunukuu mambo hayo ya msingi kutoka katika mtaala wa elimu ya sekondari ulioboreshwa mwaka 2013 kwasababu kwa sehemu kubwa yanajibu maswali mengi ambayo yamekuwa yakiulizwa na wengi.

Utaona tofauti kubwa sana na tulikotoka mfano mwaka 1967 malengo makuu ya mtaala yalikuwa ni;-

1. Kuwafunza watoto wajione kuwa sehemu ya jamii wanazoishi.

2. Elimu kupanda mbegu ya watu kuishi pamoja na kufanya kazi pamoja.

3. Elimu iwafanye watoto kujiona wote ni sawa kibinadamu na kuondoa majivuno ya kikabila, rangi, dini na elimu.

4. Kujenga stadi za kudadisi na kujenga moyo wa kujiamini.

5. Kuandaa watoto kwa kazi za maisha ya vijijini na wanaojitegemea.

Kwa vyovyote vile pamoja na matokeo mazuri ya mitaala ya wakati huo, ambayo shabaha yake kuu ilikuwa ni kumuandaa mototo kutumia zaidi rasirimali zilizomo ndani ya eneo lake tuu kwaajili ya kujikwamua kiuchumi,Lakini sasa mtaala unatakiwa kumuandaa mwanafunzi kutumia rasirimali zilizomo katika dunia kwaajili ya kujikwamua kiuchumi.

MAENEO AMBAYO NI UFUNGUO WA KUJIFUNZA (KEY LEARNING AREAS)

Mtaala hapa umefafanua maeneo ambayo mwanafunzi ataelimishwa ili aweze kupanua uelewa wake na hivyo kumfanya kuwa na uwezo wa kuamua kuchagua kuendelea na elimu ya juu na fani atakayo.Na ili kuyafanikisha hayo mtaala umetaja maeneo matano ambayo ndiyo kama ufunguo katika kujifunza nayo ni ;-

A.Lugha (languages)
B. Sayansi asilia (Natural science)
C. Teknologia (Technology )
D. Sayansi ya jamii (social science)
E. Biashara na sanaa za ubunifu (business and aesthetics)

Hapa sasa ndipo panapokwenda kujibu maswali mengi yaliyotapakaa katika jamii.Mtaala umefafanua vizuri sana kwa kuainisha kila somo litakalofundishwa shuleni na eneo linalohusika.
Tuanze na ;-

A.LUGHA;

hapa mwanafunzi atafundishwa lugha ya Kiswahili,Kiingereza,kifaransa,na kiarabu.Kupitia lugha mwanafunzi atajenga uwezo na kuimarisha mbinu za mawasiliano na kumfanya kujiamini na kukidhi mahitaji ya nchi na dunia.

B. SAYANSI ASILIA NA TEKNOLOGIA;( NATURAL SCIENCE)
Hapa mwanafunzi atasoma masomo yafuatayo

1.baiologia (Biology)
2. chemia (Chemistry)
3. Fizikia (Physics)
4. Hisabati ( Mathematics)
5 Mawasiliano na masomo ya kompyuta ( Information and Computer Studies)
6. Elimu ya ufundi ( Technical Education)
7. Kilimo (Agriculture)
8. Uchumi wa nyumbani ( Home Economics)

Kupitia masomo haya mwanafunza atapata msingi bora wa kuanza kushirikiana na mazingira yake kwa kutumia miongozo ya kisayasi na kiteknologia.Mwanafunzi ataanza kuunda bidhaa za kitecnologia kupitia mtaala huu wa elimu ya sekondari.Haya yameainishwa katika sehemu ya mtaala huo.

C. SAYANSI YA JAMII (SOCIAL SCIENCE)

Masomo yafuatayo yanahusika hapa-

1.History
2. Geography
3 Civics

Kupitia masomo haya mwanafunzi atapata nafasi ya kujifunza elimu ya uraia,yaani haki na wajibu wake,ataweza kujitambua na kuendana na jamii,uchumi, siasa, utamaduni na mabadiliko ya kiteknologia yanayochukua nafasi ndani ya jamii na nje ya jamii husika.

D. MASOMO YA BIASHARA (BUSINESS STUDIES)

Hapa mwanafunzi atapata fursa ya kujifunza masomo yafuatayo-

1.Commerce
2.Book-keeping

Katika masomo haya mwanafunzi atapatiwa msingi katika maswala ya usimamizi wa maswala ya fedha (financial Management), kupangilia (planning), masoko ( marketing), Manunuzi (purchasing), mahusiano ya jamii ( public relations) na Ujasiriamali (entrepreneurship).

E. SANAA (AESTHETICS)

Mwanafunzi atasoma masomo yafuatayo-

1. Sanaa za uchoraji,uchongaji na ufinyanzi ( Fine Arts)
2. Sanaa za maonyesho (Theatre Arts)
3. Elimu ya viungo na michezo (Physical Education)
4. Muziki ( Music)

Kupitia masomo haya mwanafunzi ataweza kujifunza mambo ya msingi ya kimaisha ikiwa ni pamoja na ya ujumla na yale ya ujuzi wa kipekee ambayo ni ya muhimu sana katika namna mbalimbali za kimaisha.Hii itawatia moyo wanafunzi kuonyesha vipaji vyao na thamani yake na kuitambua sanaa pamoja na utayari katika maisha yao.maelezo haya yametoka katika sehemu ya maelezo ya mtaala huo ulio katika lugha ya kiingereza.

Pia kuna masomo ya ziada ambayo mwanafunzi anaweza kuyasoma kufuatana na mzingira fulani kwa kadiri atakavyohitaji.Mfano wale wa shule za sekondari za ufundi wanaweza kusoma somo la ENGINEERING SCIENCE wakati masomo ya EDITIONAL MATHEMATIC, BIBLE KNOWLEDGE na ISLAMIC STUDIES, yanaweza kusomwa na mwanafunzi yeyote kutoka katika shule yeyote ya sekondari.

Kwa ufupi ukiutazama mtaala huo japo una mambo mengi ambayo sijapata nafasi ya kuyasemea lakini kwa sehemu hii tu inaonyesha kujibu maswali mengi yaliyokuwa yakiulizwa na wengi.

Wengi wamekuwa wakisahau kuwa elimu ya msingi na sekondari ni elimu ya awali inayomuandaa mwanafunzi ama kuendelea na elimu ya juu au kujitegemea.Vilevile elimu hii lazima iwe na upana katika mfumo unaokidhi mahitaji ya nchi katika kujitegemea na pia kukidhi mahitaji ya dunia.Mwanafunzi awe na uelewa wa mambo yanavyokwenda na mabadiliko yanayotokea duniani kote sio nchini kwake tu.

CHANGAMOTO ZA MITAALA NA UTATUZI WAKE

Pamoja na kwamba hatujapata nafasi ya kuuchambua mtaala wote lakini kwa ujumla kama utapata nafasi ya kuupitia wote uko vizuri.Kinachojitokeza ni changamoto tu za utekelezaji wa mtaala wenyewe.

Maeneo machache yenye changamoto za utekelezaji wa mtaala kwa sasa viko nje ya shule husika watekelezaji wa mtaala na wakati mwingine hata serikali.

Mfano mtaala unapotaja baadhi ya rasilimari wezeshi zitakazotumika katika kutekeleza mtaala utagundua vingi havitekelezeki kwa sasa mfano;-

TEACHING LOAD AND TEACHER STUDENT RATIO (MZIGO WA KUFUNDISHA NA UWIANO WA MWALIMU NA MWANAFUNZI)

Mtaala umefafanua kuwa mwalimu kwa wastani wa juu kabisa atakuwa na vipindi visivyozidi 30 kwa wiki,vipindi visivyopungua sita (6) kwa siku sawa na masaa manne (4) ya kufundisha.Mtaala unatakiwa ufafanue wazi nini cha kufanya endapo kutatokea upungufu na kufanya malengo ya mwalimu kutotimia.

Mtaala umeeleza kuwa mwalimu anatakiwa afundishe idadi ya wanafunzi 40 katika darasa moja jambo ambalo mpaka sasa halijafanikiwa.Kutokana na upungufu mkubwa wa walimu na majengo. mtaala ulitakiwa kutoa mapendekezo juu ya hatua zinazotekelezeka endapo kutatokea upungufu wa walimu.Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza tatizo lolote linalosabishwa na upungufu wa walimu,kuliko kusubiri tathmini za mwisho zitakazoamua nini cha kufanya tukiwa tumeshapoteza sehemu kubwa ya wahitimu.

SCHOOL FACILITIES (VIWEZESHI VYA SHULE)

Mtaala umejieleza kuwa rasilimari wezeshi za shule zita toka moja kwa moja selikarini,selikari za miji,na wamiliki wa shule binafsi.Rasirimali wezeshi hizo ni pamoja na;-
PHYISICAL RESOURCES (rasilimali zinazoonekana)

Pametajwa ujenzi wa madarasa,maabara,maktaba,chumba cha mawasiliano (kitakachokuwa na computer,photocopy mashine,fax,internet connection,printing mashine,scanning mashine)mabweni ,jiko na chumba cha matibabu au dispensery kwa shule za bweni.

A . MADARASA

Mtaala umetoa ufafanuzi kuwa chumba cha darasa kinatakiwa kiwe na ubao wa kuandikia , vifaa vya kukalia na kuandikia vilivyotimia.Hili bado ni changamoto na mtaala ungepaswa kutamka wazi kuwa endapo vifaa hivi havitapatikana ni njia gani mbadala inaweza kutumika, kunusuru matokeo yeyote yanayosababishwa na watoto kutokuwa na vifaa vya kukalia na kuandikia.Ninapendekeza kuwa kuanzishwe kodi maalumu kwa watu wote wanaosomesha watoto wao kwenye shule za gharama na nje ya nchi.kodi hii itumike kufidia upungufu utakaojitokeza katika viwezeshi hivyo.Pia wazazi wenye kipato cha kati walazimike kupeleka vifaa hivyo ili vilivyopo vitumike kwa wasiojiweza.Na ukizingatia zoezi hili sio la kila siku basi baada ya muda mfupi tutakuwa tumemaliza tatizo.

B.MAABARA

Maabara imeelezwa kuwa iwe imekamilika ikiwa na vifaa vyote muhimu kwa majaribio ya kisayansi.Maabara hizi hazipatikani kwenye shule nyingi na badala yake napendekeza kuwa maabara za shule jirani zitumike kusaidia wanafunzi wa shule zisizokuwa na maabara.Kuhusu gharama za usafiri kama ni mbali wazazi watachangia kama wanavyochangia kwanye mavazi nk.Hata hivyo shule zinaweza kuwa na miradi ya kujitegemea itakayochangia gharama za usafiri.

C.MAKTABA

Zimetajwa kuwepo kila shule zikiwa na vitabu vyote vya kiada na ziada.mpaka sasa shule nyingi hazina maktaba.Wananchi wahamasishwe kuzijenga kama walivyojenga shule na watu binafsi wapewe fursa ya kuwekeza kama miradi ya kimaendeleo.wanaweza kuwekeza kwa mtindo wa hisa kama mradi wa kijiji au kikundi cha uwekezaji.Watawekeza vitabu kwa kuwalipisha wanafunzi wa shule zinazowazunguka kiasi kidogo cha fedha ikiwa kwa mwaka au hata kwa siku na fedha hiyo itawawezesha kujikwamua kiuchumi.

D. MABWENI NA NYUMBA ZA KULALA WALIMU.

Hayo yametajwa na mitaala kuwa ni muhimu katika shule za bweni.changamoto iliyopo shule hizi ni chache na zilizopo haziko kwenye viwango .Ninapendekeza kuwa wanafunzi wachaguliwe kulingana na mahala wanakotoka.Na utaratibu wa kupata huduma nyingine ambazo hazipo utumike utaratibu ambao nimependekeza awali.

E.KUMBI

Imependekezwa kuwa kuwepo na kumbi zitakazokuwa zikitumika kwa shughuli mchanganyiko .Kwa shule ambazo hazina kumbi napendekeza kuwa zitumie madarasa kwa dharula.


Pia imeelezwa kuwa kumbi hizo zitatumika katika baadhi ya michezo ya ndani.Napendeleza kuwa kuwepo na darasa moja maalumu liyakalokuwa likitumika katika shughuli za michezo ya namna hii ili kukidhi hitaji la wahusika kabla ya kuwa na ukumbi rasmi.

F.VIFAA VYA MAWASILIANO (ICT FACILITIES)

Vifaa kama computer , mashine za fotokopi,scanner,internet,nk navyo vimezingatiwa katika mtaala.Ninachopendekeza vifaa hivi view ni lazima kwa kila shule kutokana na umuhimu wake. Kwa mujibu wa unyeti wa shwala husika ninapendekeza kuwepo na wazabuni watakaokuwa na mkataba na wizara ya elimu kwaajili ya kutoa huduma hii endapo shule itakuwa haina vifaa hivi.

Kitendo cha kuendelea kusubiri pasi na kuchukua hatua ya kupeleka vifaa hivi mashuleni tutaendelea kubaki nyuma kimaendeleo kwa kuwa majirani zetu watatumia mwanya wa ujinga na ushamba wetu kujinufaisha.

Kutumia vifaa hivi vya kisasa kujifunzia na kufundishia ndiyo njia rahisi zaidi ya kijipatia elimu na kuongeza uelewa.Kwa wale wenye uwezo mtaala ueleze wazi kuwa wataruhusiwa kutumia vifaa hivi sawa na kama ambavyo wazazi walivyoruhusiwa kuwanunulia vitabu watoto wao.kufanya hivyo kutajenga mazoea ya matumizi ya vifaa hivi kwa watoto na kuwafanya waongeze uwezo wao wa kuelewa.

Mtaala pia umetaja maswala kadhaa ambayo yanatekelezeka kama maeneo ya kupumzikia,michezo,vyoo kwa wenye mahitaji maalumu, vifaa maalumu kwaajili watoto wenye mahitaji maalumu nk.Kifupi ni kwamba hayo yote yanatekelezeka.mfano;-

A. Maeneo ya mapumziko na michezo

Kwa maeneo ya kupumzikia napendekeza sio lazima yawe majengo bali inaweza kupandwa miti maalumu yenye kivuli cha kutosha na kutumika kwa mapumziko.Katika michezo ninaimani kuwa shule nyingi zinamaeneo ya wazi ambayo yanaweza kutumika kwaajili ya michezo kwa utaratibu maalumu utakaopangwa na shule.

B. Vifaa maalumu kwa wenye mahitaji maalumu .

kwanza watu wenye mahitaji maalumu huwa ni wachache.Hivyo mitaala ieleze wazi kuwa kama serikari haitawapa vifaa maalumu vitatoka wapi kutokana na ulazima wake.

C. Vyoo kwa wenye mahitaji maalumu.

Napendekeza tubadilishe miundombinu ya baadhi ya vile vilivyopo kutatua tatizo la uhitaji wa watu wenye mahitaji maalumu.

Ninaimani kunamambo mengi katika mtaala wa elimu ya sekondari ambayo ni changamoto. lakini tukitumia nia ya dhati ya kuendeleza vipaji vya watoto wetu, tunaweza kutumia changamoto hizo kama daraja na kutafuta mbinu mbadala katika kutekeleza mtaala wetu.
Mfano katika changamoto ya muda wa kujifunza mtaala umeeleza kuwa mwanafunzi atajifunza kwa siku 194 kwa mwaka.kutakuwa na vipindi 40 kwa wiki sawa na vipindi 8 kwa siku.Masaa matano (5) ya kujifunza kilasiku.

Kwa hesabu za haraka muda huu ni mchache sana kujifunza .Vivyohivyo bado kunasiku dharula zinazofanya wanafunzi wasitumie muda wao vizuri kujifunza.Dharura hizo ni pamoja na upungufu wa walimu,sikukuu za kitaifa,Maradhi kwa walimu na majanga.Ninapendekeza siku ya jumamosi itambuliwe na mitaala na kuongeza siku za kujifunza walau kufikia siku 236.

Sio rahisi kutaja changamoto zote ila tuzitambue kwa faida ya kuboresha mtaala wetu.Ninaimani kuwa tukitumia mtaala kwa kuzingatia rasirimali tulizonazo tunaweza kuendeleza vipaji vya watoto wetu na kuwafanya wawe na mchango katika jamii yetu

Maoni 2 :

  1. Pia wamekuwepo watu wanaodai kuwa mambo ambayo wanafunzi Tanzania wanajifunza hayahusiani na maisha tunayoishi.Yaani wanajifunza mambo ambayo hatuyahitaji katika maisha yetu. SIJAKUPATA VIZURI KATIKA KUJIBU HOJA HII, NA HASA ULIPOHUSIANISHA NA HOJA YA SERA YA ELIMU KUHUSU UTOAJI WA ELIMU UMETEGEMEA MATAKWA YA DUNIA PIA.

    JibuFuta
  2. Tunahitaji kuzijua hizo shule zenye mitaala ya sanaa kama music

    JibuFuta