Jumatano, 5 Machi 2014

MAKOSA MAKUU MANNE WANAYOFANYA WASOMI WENGI

Kila mtu anafahamu maana ya neno msomi bila kujali analifahamu kwa kiasi gani .kifupi neno msomi linaamaana nyingi kulingana na mtumiaji amedhamiria kumaanisha nini .Wapo wanaomaanisha mtu aliyevuka levo ya shule ya high school na kuingia katika levo ya elimu ya vyuo.Wengine wanatumia neno hilo kwa mtu anayesomea ujuzi wowote kwa kiwango cha shahada na kuendelea.

Lakini msomi katika mtazamo wangu mimi ni mtu yeyote mwenye elimu au ujuzi unaoweza kuleta mabadiliko ya kifikra kwake yeye mwenyewe na kwa jamii inayomzunguka.Msomi huyu anaweza kuwa ni wa kidini au wa maarifa ya kidunia. Watu hawa wamebeba matarajio makubwa sana ya wanajamii hasa ukizingatia kuwa kunakauli mbiu nyingi zinazozungumzia elimu, mfano ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA,ELIMU NI UKOMBOZ, ELIMU NI KAZI nk.
Wasomi hawa ama kwa kufahamu au kwa kutofahamu wamejikuta wakifanya makosa kadhaa tofauti na matarajio ya wanajamii wanao wazunguka .Jamii imebaki na maswali mengi juu ya watu hawa pale wanaposhindwa kuwatofautisha na wanajamii wasiokua na kisomo kwa jina la utani ( wasiokwenda shule).Kwasababu hiyo imefikia hata baadhi ya watu kutoona umuhimu wa kijielimisha kwa kutoshawishiwa kwa namna yeyote pale wanapoona matokeo ya maisha ya hao wanaoitwa wanakisomo.

Makosa yanayofanywa na wasomi wengi ni kama ifuatavyo:-

1. HUSUBIRI MPAKA WAMALIZE SHULE AU CHUO NDIPO WAANZE KUTUMIA UJUZI WALIOPATA.
Fikra za binadamu kwa kawaida hazihitaji kujazwa ujuzi mfano wa unavyoweza kujaza upepo kwenye mpira wa baiskeli ili iweze kutembea.Kama ingelikuwa hivyo basi mpaka leo kusingelikuwa na mwalimu hata mmoja duniani na badala yake sote tungekuwa ni wanafunzi  wa milele tena maisha yengekuwa ni kitu kisichotekelezeka kwa kukosa ujuzi.

Nataka nikukumbushe kuwa ujuzi huja kwa njia ya wazo mfano wa cheche ndogo sana katika fikra zetu kupitia walimu ,vitabu,maonyesho,kufikiri,kutafiti,kujaribu nk.Hili wazo changa hukuzwa na muhusika pale anapoamua kulifanyia kazi; akifanikiwa huleta mabadiliko ya jinsi alivyokuwa akifikiri na mabadiliko hayo ndiyo mchango katika jamii inayomzunguka.

Kwa wasomi wengi waliotuzunguka wamekuwa hawana mchango wowote katika jamii japokua wana utitiri wa mawazo machanga katika fikra zao walizopata kupitia walimu, vitabu, semina, wasomi wenzao, majaribio ,tafiti nk. Walio wengi katika kundi hili huendelea kusubiri mpaka wamalize mafunzo ndipo waanze kufanyia kazi michango ya mawazo waliyoipata. Lakini kwa bahati mbaya kwakuwa mawazo wanayopata ni mengi na kwa muda mrefu hivyo mengi husahaulika na kutupya nje ya fikra na matokeo yake elimu ile huwa haina mchango wowote kwake mwenyewe na wala kwa jamii.

Kwasababu hiyo msomi huyu atakapomaliza mafunzo yake atajikuta akifanywa mtumwa na hao wasiokuwa wasomi kwasababu walikubali kutumia walau cheche moja tu ya wazo kubadilisha fikra zao na kuleta mabadiliko tunayoyaona.

Historia ya mabingwa wengi katika Nyanja mbalimbali za kisayansi, kilimo na maeneo mengine waliobuni fomula na vitu vingine mbalimbali tunavyotumia leo katika maisha yetu, hawakujifunza kokote, bali walitumia cheche ndogo sana za mawazo yaliyobadilisha mitazamo yao na kujikuta wakipata matokeo ambayo hata wao wenyewe yaliwashangaza. Na kwasababu hiyo tunaweza kujua mambo makubwa hata yaliyo mbali kiasi gani kwakuwa wapo watu waliotumia mawazo madogo sana kutoa ufumbuzi wa matatizo makubwa.Naam hii ndiyo kazi inayotarajiwa kufanywa na msomi yeyote Yule.

Ninapenda kuwashauri mnaoitwa wasomi kuamua kutumia kila wazo mnalolipata kuleta mabadiliko katika jamii na kuepuka kudanganywa na baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema kwa kuwaambia " huwezi kwa kuwa elimu yako ndogo,hujafuzu,nk".Tumia mawazo uliyoyapata kuleta mabadiliko na uwe na mchango katika jamii na sio kusubiri mpaka ukabidhiwe cheti kwa kuwa cheti chako kitakaa kabatini na wewe ndiye unayehitajika na jamii.

Ona haya kwa watu wasiokuwa na elimu kubwa kama ya kwako wanapokuwa na mchango mkubwa katika jamii kwa kuamua kutumia mawazo finyu sana, tofauti na wewe uliyepata fursa adimu kabisa ya kukutana na watu mbalimbali waliobobea katika Nyanja mbalimbali za kiujuzi na kukushirikisha mawazo yao.Amua leo kuanza kutumia kidogo ambacho tayari unacho ukikikuza kutoka katika fikra zako za ndani na sio kusubiri kukaririshwa kama kasuku. Maisha sio risala unayoweza kuisoma kwa mgeni rasmi na kutupwa baadaye bali ni vitendo vya kila siku na vitendo hutoka ndani ya fikra na fikra hutokana na cheche ndogo za mawazo na cheche za mawazo hutokana na kujifunza pamoja na kufikiri.

2.HUWA HAWEPENDI KUJIFUNZA KUTOKA KWA WENGINE

Kujifunza kutoka kwa wengine ni jambo lisilo epukika . Ila kwa kutokujua ama kwa kujua wasomi wengi wamekuwa hawapendi kujifunza kutoka kwa wengine kwa kigezo kuwa elimu yao inawatosha.

Unachotakiwa kufahamu ni kwamba kutoka kwa kila mtu tunayekutana naye awe ni msomi ama sio msomi kunakitu cha kujifunza .Unaweza kuwa msomi wa digrii mbili lakini siku moja ukapelekwa katika mapori ya karibu na Serengeti na kujikuta ukikaa nyuma ya morani wa kimasai asiyejua hata “a” inaandikwaje kwa hofu ya kutojua nini cha kufanya mara utakaposikia muungurumo wa simba.Vivyo hivyo pamoja na usomi wowote unaoweza kuwa nao lakini ukajikuta ukimshangaa mototo wa miaka saba aliye kariri ukurasa mzima wa biblia au msahafu na kuusoma bila kutazama kokote tena mbele ya hadhara kitu ambacho ukiambiwa wewe hata paragrafu moja huijui.Wakati mwingine unaweza kujikuta ukishindwa kuamini macho yako pale ambapo utamkuta mama wa nyumbani asiyekuwa na elimu yeyote ya biashara akiuza mbogamboga au bidhaa anazotengeneza kwa mikono yake mwenyewe nje ya nchi.

Kutoka kwa kila mtu tunayekutana naye kuna wazo kuu linaloweza kufaa kwa maisha yetu, chamsingi ni kumtazama kwa mtazamo chanya ukiwa na lengo la kupata kitu kutoka kwake.

3. KUISHI MAISHA YA KIMAONYESHO

Haya ni maisha yanayozingatia utambulisho wa mtu tu (personal presentation) na si kwaajili ya matokeo ya kuwepo kwake katika jamii. Wasomi wengi wanapenda maisha haya ya mionekano na utambulisho ulioambatana na sifa za kuwa na kiwango cha juu cha elimu. Wamejizatiti katika kukariri nadharia ili kufaulu masomo.Wakati mwingine huandaa nyaraka (documentation) na kuziwasilisha mahala Fulani Fulani ikiwemo katika mitandao kwa makusudi ya kuajiriwa, kujenga utambulisho zaidi na kuheshimiwa zaidi na sio kuleta majibu ya maswali mengi yaliyomo katika jamii. Hujisikia fahari kuteuliwa kuwasilisha risala (speech presentention) ambayo hakuhusika hata kuchangia neno moja la kiutafiti ndani yake.  Kupitia haya ndipo kumezuka migongano ya mawazo kwa wanajamii kwa wengine kutotambua mchango wa elimu na hivyo kutoona umuhimu wake.

Pia kutokana na udhaifu huu wa kutafuta utambulisho imesababisha baadhi ya wanakisomo hasa wale walioko vyuoni kutorejea na mchango unaokusudiwa na jamii na badala yake ndiyo wamekuwa matapeli wa kutupwa,walaji na wauzaji wakubwa wa unga (madawa).Wakiwa vyuoni badala ya kutoa mchango wa kuleta mabadiliko katika nchi wanakuwa walalamikaji namba moja na vinara wa kuendesha migomo na maandamano ya madai ambayo hayana tija ya moja kwa moja kwa jamii.

Ninapenda kuwakumbusha wasomi wote kuwa ,ninyi ndiyo mliopokea michango ya mawazo kutoka kwa watu wengi, hivyo mnafanana na mtu anayemrushia jiwe nyoka akiwa juu ya kilele cha mlima yaani mna (potential energy). Sote tunafahamu kuwa kufanya hivyo ni tofauti na anayerusha jiwe kwenda juu ya mlima hasa linapokuja swala la matokeo.

Kama wewe unasomea uchumi tambua kua tangu sasa wewe ni mchumi hivyo ishi maisha ya mchumi,jenga uchumi,fundisha uchumi, endeleza uchumi nk. Kama unasomea kilimo tangu sasa wewe ni mkulima ,onyesha maisha ya mkulima ,lima,elekeza kilimo,kuza kilimo nk. Vivyo hivyo kwa mwanamahesabu fundisha hesabu,rahisisha hesabu kwa jamii,buni hesabu,endeleza hesabu. Mwanasheria,simamia sheria,tunga sheria,tafiti sheria,tetea sheria,badilisha sheria,fundisha sheria,nk.Mwanasoshologia ,Daktari,mwanafizikia,mwanajiografia,mwanaikologia,mwanasaikologia nk . Sitaweza kuwataja wote bali kilammoja kwa upande wake fanya unachosoma au ulichosoma ukitumia mawazo machache uliyoyapata na kuyakuza katika fikra zako ili kuleta mabadiliko bila kujali levo yako ya elimu.

4. KUJIFANYA WA KISASA KULIKO UHALISIA WENYEWE
Shida nyingine inayowakumba wasomi ni kutaka kuishi maisha ya kisasa zaidi ya uhalisia ulivyo.Tatizo hili ni la kidunia hasa kwa vijana ambao wanategemewa kutoa mchango wa muda mrefu katika jamii.
Wasomi badala ya kutumia mawazo wanayopata katika mashule na katika vyuo kuleta maendeleo au mabadiliko wao wanatumia muda mwingi kushughulika na swala la fasheni.
Ikumbukwe kuwa swala la fasheni ni la kimaumbile yaani ni asili ya binadamu kupenda kutumia mitindo mipya ya kimaisha ili maisha yawe na ladha.Lakini si kila fasheni ni salama kwa maisha ya binadamu.

 Unapaswa kufikiri kuhusu mitindo mipya inayojitokeza kama ya kubadilisha viungo iwe kuvipunguza au kuviongeza ,michoro ya mwilini, starehe za usiku, mavazi ya utupu, picha chafu nk .Mambo haya yamekuwa ni maarufu sana katika makusanyiko ya wasomi na matokeo yake wengi waliokwenda kupata elimu wamerudi na fasheni badala ya kile walichokusudiwa kurudi nacho ( yaani ujuzi wenye tija).

Mabadiliko haya ya kidesturi yamewafanya baadhi ya wasomi kushindwa kuchukuliana au kutoendana na jamii husika hivyo kushindwa kushirikiana nayo pale wanapogundua kuwa wako tofauti sana na jamii zinazowazunguka.Mfano wasomi wamekuwa na desturi za kiwango kipya sana kulinganishwa na jamii husika kuanzia wanavyo VAA (mavazi yao yanastaajabisha),KULA( wanakula vyakula visivyojulika na jamii),KUWASILIANA (wanatumia lugha isiyojulikana na jamii na njia isiyozoeleka kwa jamii mfano hupenda kutumia technologia ya mawasiliano ambayo ni mpya sana kwa wakati huo),MAKAZI (hupenda makazi yaliyojitenga yasiyochangamana na wanajamii wa kawaida) UZAZI (hawapendi kuzaa hata wakizaa hawapendi kukaa na watoto) USAFIRI (hawapendi kutumia usafiri wa umma) MIJUMUIKO (huanzisha jumuiya (communities ,associations) zao zinazotetea maslahi yao na si ya jamii inayo wategemea) .
Kwa namna yeyote utaona kuwa kitendo cha kujifanya wa kisasa kuliko hali ilivyo huwafanya wasomi kujitenga na jamii bila kupanga (atomaticaly) na kujikuta wakiwa hawana ushirikiano na jamii hivyo kutokuwa na mchango wowote

Wosia wangu kwa wasomi ni kwamba ,"tambua nafasi yako katika jamii na epuka kuwa wa kisasa zaidi kuliko hali ilivyo ukawatenga ndugu jamaa na marafiki na kuwafanya kutotambua mchango wako" .Kaa katika hali ya kimwingiliano na jamii ili ulete mabadiliko haiyamkini kwa mawazo machache utakayoyapasia kwa wachache yatazalisha fikra zitakazoleta mabadiliko makubwa kuliko unavyofikiria.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni