Alhamisi, 27 Machi 2014

JINSI YA KUTAMBUA KIPAJI CHAKO



kama kuna swali ambalo linahusu maisha binafsi ya mtu na limekuwa na majibu hafifu sana ni swali       linalohusu kipaji.Kuna idadi kubwa sana ya watu wanaomaliza maisha yao hapa duniani bila kufahamu ni aina gani ya kipaji walichonacho.

Wengine hata hawaamini kuwa wanaweza kuwa na kipaji.Kwa sababu hiyo wamefikiri kuwa kipaji ni kwa baadhi ya watu tu na swala hili haliwahusu hata kidogo.Fikra hizo sio za kweli  hata kidogo na ningependa nikueleze wazi kuwa hata wewe unakipaji cha pekee sana.Nasisitiza tena kuwa hata wewe una kipaji Ila hujakitambua na hujakitumia.Kupitia  hii ndiyo itakuwa nafasi yako ya kuanza kufaidi matunda ya kipaji chako.


Acha kujivunya moyo kuwa umri wako umepita na huhitaji tena kusikia habari ya kipaji au habari ya kipaji ni kwaajili ya watoto wadogo tuu.Kitabu hiki kitakupa mwongozo wa kubadili mwelekeo wako katika kutumia kipaji chako bila kuathili maisha yako.

MAANA YA KIPAJI
N
eno kipaji sio neno geni kwetu hasa sisi tuliozaliwa katika miaka ya hivi karibuni.Limezoeleka sana kutokana na kuzungumzwa sana katika maeneo mbalimbali siku hizi .Chakusikitisha ni kuwa, Jinsi kipaji kinavyotamkwa ni tofauti kabisa na kinavyotumika.Kwa usemi mwingine naweza kusema kuwa kipaji kinatamkwa sana kuliko kinavyotumika.Swala hili linafanya maana ya kipaji kupotea na hivyo jamii kuishi bila kutumia nyenzo hii muhimu ya asili. IF YOU RECOGNIZE YOUR TALLENTS, USE THEM APPROPRIETLY, AND CHOOSE A FIELD THAT USES THOSE TALLENTS ,YOU WILL RISE TO THE TOP OF YOUR FIELD (Kama ukitambua vipaji vyako, vitumie kwa usahii na uchague eneo linalotumia vipaji hivyo, utainuka juu kabisa ya eneo lako).Hii ni kwa mujibu wa nukuu kutoka kwa  Ben Carson  kama alivyoandika katika kitabu chake cha think big.

Bila kujali ni kipaji cha aina gani. kipaji ni uwezo au nguvu za asili anazokuwa nazo binadamu katika kutenda jambo Fulani kipekee bila kujali kiwango cha ujuzi alionao.Uwezo huu unaweza kujitokeza katika kufikiri ,kutamka, kutenda, kuhisi nk.

kipaji si ile shughuli tuifanyayo bali ni ule uwezo wa asili tunaozaliwa nao na kujijenga ndani yetu kuwezesha kufanya aina flani ya shughuli au kitendo kwa namna ya upekee sana kuliko watu wengine.Uwezo huu huwa ndiyo mfumo asilia ndani ya vinasaba vya mtu ambao hauwezi kubadilishwa kwa kuzoelea kufanya mambo flani flani yasiyoendana nao.


kwa mimi ninayeamini uwepo wa mungu nasema hii ni zawadi ya pekee kwa kila binadamu kutoka kwa Mungu na kila mtu amejaliwa kwa namna yake ili sote tufaidiane.

DALILI ZA KUANZA KUONEKANA KWA KIPAJI

Mara nyingi vipaji vingi ambavyo ndiyo uwezo uliomo ndani yetu kuwezesha kufanya mambo kadhaa kiupekee,  huanza kugundulika wakati muda umeshapita sana.Sababu kubwa ya kutogundulika haraka kwa vipaji hivi (uwezo), ni kutokana na kipaji kujitokeza kwa namna ya mficho.Hujitokeza kwa mfano wa faili lililofungwa na kuandikwa kwa nje  uwezo wa michezo ,taaluma,ubunifu,au uimbaji bila kufafanua ni uwezo wa mchezo upi hasa au taaluma ipi au ubunifu wa nini au uimbaji wa aina gani. lakini kwa bahati mbaya ufafanuzi huo ni mpaka ufungue ndani.Kwasababu hiyo hata wengi wa wanavipaji huishia kutumikia anwani za mafaili hayo mpaka wanakufa. Wanatumikia michezo wasijue uwezo wao ni juu ya mchezo gani hasa, wengine taaluma wasijue ni taaluma gani na wengine uimbaji wasijue uimbaji wa aina gani.

Kitu ninachoomba ukitambue ni kwamba kipaji huanza kwa namna ya wazo.Wazo hili huwa halisomeki sawasawa kama ilivyo kwa faili lisilo na ufafanuzi . Nalo hukuwa taratibu kwa kadiri mtu huyu anavyochukua hatua au kulifanyia kazi. Kwa maana nyingine ningesema kulifanyia mazoezi.Mfano; kama wazo likiwa ni uwezo wa kitaaluma basi haliwezi kujitokeza na kujiweka wazi mpaka utakapochukua hatua ya kusomea au kufanya kazi katika taaluma hizo ambazo ule uwezo wako wa asili (kipaji) unajipambanua.

Kupitia shuleni huwa ni rahisi kiasi kwasababu watoto hupewa uwanja mpana kidogo wa kujaribu kuonyesha japo vipaji vichache, haswa vya kitaaluma chini ya uangalizi flani. Lakini cha kusikitisha ni kwamba hata mashuleni bado  nafasi hiyo ni finyu sana kuonyesha na kukuza vipaji vyote vilivyopo duniani.Vinavyokosa nafasi hiyo ni vile ambavyo viko nje ya mitaala kutokana na kutovitilia maanani hivyo kutengwa na mfumo wa elimu.

Katika maeneo maalumu ya kukuzia vipaji imekua rahisi kuvigundua.Kwasababu watoto au wanafunzi hupewa nafasi ya kuonyesha wanachokiweza na kisha kuwaweka katika makundi maalumu.Ni wajibu wetu kuendelea kuanzisha vituo hivi na kuwatia moyo wanaofanya hivyo. Lakini tufikirie kuanzisha vituo vitakavyoshughulika na aina nyingi za vipaji na sio aina moja tu ya kipaji kama ilivyo sasa. Kwa kuwa  vituo vingi vinaendeleza vipaji vinavyoendana na michezo.

NANI ANA KIPAJI
Ukweli ni kwamba kila mtu ana kipaji cha peke yake  ambacho kinamtambulisha yeye na kumfanya awe na mchango wa tofauti na mtu mwingine yeyote duniani.Kosa kubwa tunalolifanya ni kwamba wengi tunaishi kwa kufuata na kuigiza vipaji vya watu wengine.Inawezekana ikawa ni wewe na pengine umefanya hivyo bila kufahamu.

kwa maana nyingine ni kwamba watu wengi wanaishi kwa kutumia uwezo ambao haumo ndani yao.Wanafanya shughuli ambazo haziendani na mfumo halisi uliojengwa  ndani yao.Wanaenda kinyume kabisa na namna mfumo wa  ubongo wao,ufahamu wao,na miili yao ilivyosukwa

AINA ZA VIPAJI
Kama laiti tungeambiwa tutaje aina zote za vipaji basi ilibidi tuitishe jopo la watu watakaofanya kazi ya kuorodhesha vipaji.Ingebidi kurasa kwa kurasa zitumike ndipo tufanikiwe kutaja vipaji vyote.Hata hivyo kuna vipaji vingine ambavyo bado havijatokea navyo vimekosa fursa hiyo. Kwasababu ya kwamba wenyenavyo hawajazaliwa au mazingira hayajaruhusu vianze kufanya kazi.

Kama utakuwa makini sana utagundua kuwa kila aina ya kipaji ni cha pekee sana Hata kama wanavipaji unaowatazama watakuwa na kipaji cha aina moja. Chukulia umepewa zoezi la kuwatofautisha waandishi wa vitabu kumi kupitia vitabu vyao.Kwa namna ya ajabu sana hata kama wote watakuwa na kipaji cha uandishi wa vitabu. Hakuna siku watajikuta wote wameandika kitu kinachofanana kwa 100%, hata kama wazo litakuwa moja.Watatofautiana katika matumizi ya vitenzi ,hadithi,misemo,falsafa,nk, na kwasababu hiyo kila mmoja ataoneka ni wa tofauti na mwenzake .

Vipaji hivi Kwa mtazamo wangu nimevigawanya katika makundi kadhaa ili kurahisisha kupata uelewa wa jumla maana sio rahisi kuvitaja vyote.

Vipaji vya taaluma zote za sayansi asilia ,teknolojia na sayansi  ya kijamii.
Hapa pana vipaji vinavyomuwezesha mtu kufanya shughuli mbali mbali za kisayansi ikiwa ni ile asilia au ya kijamii. Kuna shughuli nyingi sana zinazoingia moja kwa moja katika kundi hili kwa kutaja baadhi ni:-
Hisabati,fizikia,kemia,biologia,jiografia,historia,lugha,uhandisi na ufundi wa aina zote.Pia utengenezaji wa program za kompyuta,kutumia vifaa vya kielekroniki kama kompyuta nk,ubaharia,uandishi wa vitabu na habari,uhariri wa vitau na habari,uchumi,takwimu,kilimo,uvuvi,ufugaji,uwindaji, sayansi ya tiba,uuguzi, sayansi ya anga,shughuli za maabara,sayansi ya viumbe aina zote ikiwamo vile vya bahari,mwitu na majumbani.Hata hivyo kuna uongozaji wa ndege,meli,udereva,uendeshaji pikipiki na baiskeli,

Vingine ni ualimu,utawala,uongozi,diplomasia,siasa,sheria,saikolojia,filosofia, uhubiri wa dini,ushauri nasaha,ulezi wa yatima,utunzaji mazingira,utunzaji kumbukumbu,ukutubi(maktaba)

Sio hizo tuu bali kuna shughuli nyingine za kisanii (sanaa) kama filamu,maigizo,muziki na uimbaji,ngoma za asili,usimulizi,utunzi wa hadith,uandishi wa filamu,uchekeshaji,uchoraji wa katuni na utengenezaji wa katuni za video,uhunzi,ufinyanzi,ususi,uchoraji,uchongaji,utarizi,

 Vipaji vya michezo
Hivi ndivyo vipaji vinavyomwezesha mtu kufanya shughuli za michezo mbalimbali kama ,
Mpira wa miguu,kikapu,pete,wavu,kudansi,sarakasi,mbio,kuruka kamba,ndondi,karate,bao,karata,gemu za video nk.
 vipaji vya kibiashara
Hivi ni vipaji vyote vinavyomwezesha mtu kufanya kazi zote zinazohusiana na biashara.Vipaji hivi humuwezesha mtu kufanya shughuli kama, Ujasiriamali,biashara,uwekezaji,uchuuzi,uandishi wa mchanganuo wa biashara,utunzaji wa fedha nk.
 Vipaji vya kimaumbile na hisia



Vipaji hivi Ndiyo lulu ya binadamu kwa kuwa vinatenda kazi ndani ya binadamu kuliko vinavyoonekana kwa nje.Nimeshindwa kuvipatia jina muafaka hivyo nimevipa jina la vipaji vya kimaumbile na hisia.Hapo nina maana kuwa tunavitambua zaidi kupitia maumbile na hisia za mtu husika kuliko zile shughuli anazozifanya. Licha ya kujitegemea vyenyewe mara nyingi husaidia hata vipaji vingine kufanya kazi sawasawa.

JINSI YA KUTAMBUA KIPAJI CHAKO
Niliwahi kuizungumzia mada hii ndani ya kipengele cha jinsi ya kutambua kipaji chako, katika mada inayosema nifanye nini kabla ya kujiendeleza kielimu?
 Lakini hapa nitakizungumzia kipengele hiki kwa engo tofauti kidogo ili kupanua uelewa zaidi.

Kama nilivyoeleza katika kipengele kimojawapo kilichopita kwamba kipaji hata na vitu vingine ndani yetu hujengwa vikianzia na wazo.Huu ndiyo mfumo rasmi wa maumbile ya binadamu. kwamba kilakitu ndani yetu hujiumba kupitia namna ya mawazo yasiyo wazi sana katika ufahamu wetu.Nayo hukuwa taratibu na hatimaye huwa dhahiri hata tukashiriki kikamilifu katika kuyaendeleza.

  Mtu mwenye kipaji kisichoendelezwa kwa kupewa au kujipa fursa ya kukifanyia kazi hana uwezo wa kukitambua.Hali hii ndiyo iko kwa watu wengi duniani.Ya kuwa wanavipaji ambavyo havikuwahi kupewa fursa ya kufanya kazi ili vijidhihirishe .Namna hii huwafanya kukosa hamasa ya kufanya zaidi na hivyo kilakitu kwao huwa kigumu au hakiwezekani.
Niwe muwazi kwa kusema kuwa kipaji sio ndoto kama tulivyozoea kufikiri.Bali ndoto inatakiwa ije baada ya kutambua kipaji.Mara nyingi tumezoea kuwauliza watoto wadogo watueleze ndoto zao na kuchukulia kuwa hivyo ndiyo vipaji vyao.Hapo tunakuwa hatuko sahihi hata kidogo.Mtu yeyote anaweza kuwa na ndoto ya kitu chochote au ya kuwa mtu yeyote lakini si kipaji.Nina maana kipaji hakiwezi kuja kwa kukitamani tuu.kwasababu ni kitu ambacho kipo ndani yetu tangu tunazaliwa kila mmoja kwa namna yake.Sio ajabu mtoto akatamani kuwa komandoo na akawa na ndoto ya kuwa komandoo kwasababu tu siku moja aliangalia filamu ya John comando na akaifurahia.

Kipaji hujijenga chenyewe ndani ya binadamu bila kukijengea picha yeyote.Ni uwezo wa kiasili wa kuzaliwa nao na sio wa kuhamasishwa.Hautokani na mambo yaliyokwisha kuwapo bali ni uwezo wa kipekee sana anaokuwa nao binadamu aidha katika kutenda,kuhisi,kufikiri au kusema.Kila mtu anatofautiana na mwenzake kwa uwazi kabisa hata kama wako katika kundi la kipaji cha aina moja.
Unaweza kukitambua kipaji chako kwa kuzingatia yafuatayo:-

v Wazazi au walimu wako wameshawahi kugundua uwezo wako wa jumla katika kipaji cha jumla mafano taaluma,michezo,kuzungumza,nk? Ulishawahi kujulishwa au kupata tetesi?mpaka sasa kipaji hicho kimesha jitokeza na kukufanya uwe na mahala pamoja unapofanya vizuri zaidi ? kama ndiyo tumia fursa hiyo kipaji kitatokeza.

v  Angalia mazingira ya unachofanya kama yalitokana na uwezo wako wa asili au ulijiingiza kwa kuhamasishwa na mtu,shida, au tamaa ya kutajirika haraka.Tafuta kile kinachotokana na uwezo wako wa asili ili kipaji chako kiweze kufanya kazi.

v  Angalia kama kuna ulichokuwa ukikifanya hapo zamani ambacho hata kama hukukifanya kwa ufanisi kwa kukosa maarifa lakini kilikupa upekee .Lakini kiwe kilitokana na uwezo wako wa asili na ulifanya mara kwa mara.Kiendeleze na baada ya muda kitakupa mwelekeo wa wapi uende na hivyo kufanya uwe tofauti na wengine.

v  Angalia kama unavyovifanya sasa hata bila kutumia maarifa mengi kimojawapo unakifanya kwa ufanisi mkubwa kuliko vingine vyote na kwa upekee.Hicho unachokifanya vyema zaidi ndicho kipaji chako usikidharau ukikikuza kila mtu atakiheshimu.Hata huheshimika kwa nyumba ni baada ya kumalizika ujenzi, katika msingi mtu yeyote anaweza hata akajisaidia haja ndogo.

v  Angalia katika unavyovifanya au ulivyovifanya ni kipi kilikutambulisha au kinakutambulisha na kukufanya ukubalike kipekee na sio kutokana na kiwango chako cha kisomo.Kipaji halisi hakitegemei kiwango cha kisomo, bali uwezo wa asili ndio hutawala katika kutenda jambo.Katika kiwango chochote cha elimu bado uwezo wa asili utachukua nafasi na kutawala katika utendaji na kukufanya wewe ndiyo upate sifa na sio elimu yako.

v  Jiulize kama umeshawahi kuambiwa unakipaji? Je ni kipaji gani? Umeshawahi kuambiwa mahala kwingine na hapo maneno kama hayo? Hicho ndicho unachokifanya mara kwa mara kwa ufanisi kuliko vingine?.

v  Angalia kama unachofanya unahisia nacho au unafanya kwasababu hauna kazi nyingine? Na hisia zako za ndani zinasemaje? Jali zaidi hisia zako za ndani sana zinazo husiana na uwezo wako bila kujali vitisho kwa sababu kipaji kinanguvu kuliko kitisho chochote kilichoko mbele yako.

v Orodhesha kwa umakini mkubwa mambo yote unayojikuta ukiyafanya bila hata kushurutishwa hata kama ni madogo.Tenga yale unayoyafanya kutokana na hisia mfano huruma, upendo,kuvumilia mateso ya mwili nk.Kisha yale yatokanayo na umbo lako mfano usafi,urembo nk.Utafanya hivyohivyo kwa yale unayoyafanya kwa kuzungumza,kufikiri au kivitendo.Hapo ninamaanisha  mambo kama kuandika,kuchora,kucheza,kuzungumza katika halaiki,kuhubiri dini,kubuni vitu mbalimbali,kusimamia biashara,ususi  nk.Kipe maksi kila kimoja kulingana na mara nyingi unavyokifanya.

Jiridhishe kuwa unachokipa maksi nyingi ndicho ambacho umekuwa ukikifanya mara nyingi zaidi.Kisha kichague kile ambacho umekuwa ukikifanya kipekee zaidi na kuanza kukiendeleza. Hicho ndicho kinatokana na kipaji chako.

Kama wewe hujawahi kuhisi au kusikia chochote kuhusu kipaji chako basi ni kwasababu ya kukosa nafasi ya kukionyesha.Fanya kila unachohisi kinatokana na uwezo wako wa asili hata kama kimewahi kufanywa na mtu mwingine.Pima matokeo ya mara kwa mara kwa jinsi unavyoridhishwa wewe mwenyewe,wanao kuzunguka,wanaokuongoza nk.Ni dhahiri kuwa kipaji chako ndicho kitakachokutambulisha zaidi kuliko kitu chochote.Mpaka hapo utakifahamu kipaji chako.

Maoni 5 :

  1. Somo nimelielewa Sana, mathalani Mimi hapa ninahisi ninakipaji cha uandishi wa nukuu, huw sometimes nafikiria zengine nanukuu kutok kwa watu mbalimbali. Sa sijajua hii inaweza kuwa ndo kipaji changu au.

    JibuFuta
  2. Eeh Bwana eh Mwanangu, upo vizuri, nimeipenda somo lako nimejifunza kitu, na kwa article yako nimeshatambua kipaji changu, asante mtaalam.Hata kama wadau hawatakupatia comments nyingi, upo vizuri, ubarikiwe.

    JibuFuta