Ijumaa, 8 Agosti 2014

HIZI NDIZO FAIDA ZA USOMAJI WA VITABU NA MAANDISHI MENGINE


Katika mada ya JINSI YA KUSOMA KWA KUELEWA NA KUFAULU nimeeleza kwa upana kuhusu usomaji unavyoweza kubadilisha fikra zako kwa kukupatia mawazo mapya (bofya mada hiyo kusoma).Ni dhahili kuwa kuna tofauti kubwa sana kati ya mtu anayesoma mara kwa mara vitabu na maandishi mengineyo na Yule asiyesoma kabisa.Tofauti yenyewe utaipata pale wanapo zungumza,tenda au kuamua jambo fulani.Bila shaka kila mmoja atatenda,kuzungumza au kuamua kulingana na uwingi wa taarifa alizonazo katika fikra zake na hasa hasa kama taarifa alizonazo ni sahihi.

LENGO KUU LA KOSOMA VITABU NA MAANDISHI MENGINE

Kifupi naweza kusema ni kujipatia mawazo mapya hivyo kujiongezea ukubwa wa maktaba ya taarifa katika fikra zetu.Kila mtu ana maktaba katika ufahamu wake; ukubwa wa maktaba hiyo hutegemea na uwingi wa taarifa zilizokusanywa na mtu husika.

FAIDA ZA USOMAJI WA VITABU NA MAANDISHI MENGINEYO

Faida ni nyingi sana ila nimefanikiwa kuzitaja chache na muhimu.Usomaji wa vitabu na maandishi mengine UNAWEZA:-

1.UTAKUSAIDIA KUFANYA MAGEUZI YA KIFIKRA AMBAYO KILA MTU HUYAPITIA

Kila mwanadamu ili awe na manufaa kwake mwenyewe na kwa jamii inayomzunguka, lazima apitie mageuzi ya kifikra.Mageuzi haya ndiyo yale yanayofanya binadamu awe tofauti kabisa na vile alivyokua mwanzo na kumnufaisha yeye, kizazi kilichopo na kinachokuja.Kwa sehemu kubwa mageuzi hayo hufanywa bila kupangiliwa yaani (AUTOMATICALLY) ikitegemea na aina za taarifa zinazoingia katika ufahamu wake.Maana yake ndiyo kusema LETE TAARIFA TULETE MAGEUZI, ACHA KULETA TAARIFA TUBAKI KAMA TULIVYO. 


Taarifa nyingi ziko katika vitabu,majarida,makala,matamko ya kiserikari,katika mitandao nk.Hivyo ni muhimu kuchangamkia taarifa hizo ili kupitia hizo tuleta mageuzi ya haraka katika maisha yetu. 

2.  KUKURUDISHA KWENYE NAFASI YA MALENGO YAKO MAKUU.

Nafikiri kuwa kila mtu ana malengo makuu katika maisha yake, Iwe kwa kupangilia au bila kupangilia.Maana yake ni kuwa hata kama hukupanga kuwa na malengo makuu basi mwenendo wa maisha utakupangia malengo makuu.Kilichopo ni kwamba wengi wetu hatujawahi kupata nafasi ya kuainisha malengo yetu makuu na kuyawekea mipango  mahususi.Kufuatia hilo mwenendo wa dunia umetupangia malengo makuu.

Kwa walio wengi malengo makuu yamekuwa yakibadilika badilika kwa kadiri maisha yanavyobadilika.Mfano kama mtu amekuwa hana wazifa wowote serikalini,  anaweza kuweka malengo ya kutafuta wazifa huo na kuutumia kusaidia watu wanyonge.Mara aupatapo na kujiona anaweza kuamua lolote na akasikilizwa, malengo makuu yanaweza kubadilika na kuwa kudhulumu wanyonge haohao ili kuwa tajiri.

Kwasababu hiyo kupitia vitabu na maandishi mengine inaweza kuwa ni njia bora ya kuyafikia malengo makuu katika maisha.Pia inaweza kuwa ni njia bora ya kupata elimu ya kujipangia malengo makuu au kurejea kwenye malengo hayo.

Mfano kama wewe ni msomaji wa vitabu vya dini, katiba na sheria,hutahitaji tena matamko ya Rais na viongozi wa serikali kuhusu haki za binadamu.Wala hutahitaji daktari akutembelee nyumbani kwako kukukumbusha kanuni za afya kama utakuwa tayari umeshasoma majarida yanayohusu kanuni za afya bora.Kwa wale wanaopenda kujiendeleza kielimu hawatakuwa na wasiwasi wa kupotoshwa kuhusu kozi wanazochagua kusoma, kwa kuwa watakuwa wanauelewa mpana kuhusiana na hatima ya fani wanayochukua.

Kwa vyovyote vile usomaji utakupa taarifa nyingi zinazohusiana na kile unachokikusudia au unachofanya  maishani na namna unavyoweza kukifanikisha; haiamkini pamoja na mifano ya watu waliothubutu. Usahihi ulionao na upotofu ulionao utajipambanua pale tu unapopata taarifa sahihi kuhusu mahala ulipo na njia unayoitumia kufikia lengo lako kuu.Kumbuka kufunga goli si bidii tu ya kucheza bali ni pamoja na  kufuata sheria za mchezo na unavyojielekeza kwenye goli .Vitabu vinanafasi kubwa ya kukuonyesha sheria za mchezo na namna ya kujielekeza kwenye goli .Hayo na mengine mengi unayapata kupitia vitabu na maandishi mengine.

3. KUKUFANYA KUA MTU HALISIA
Njia rahisi ya kuishi maisha halisi ni pamoja na kusoma vitabu.Mtu anaweza kujiuliza unawezaje kuishi maisha halisi kwa kusoma vitabu?.Kumbuka kuwa ,kuna dazani ya watu leo wanaoishi maisha ya kukopi tu kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi na muhimu kwa maisha yao.Bila shaka umeshawahi kumwona daktari anayemtibu mtu aliyeathirika na sigara angali kuwa yeye mwenyewe ni mvutaji wa sigara na ameshindwa kuacha. 

Wakati mwingine unaweza kumwona kiongozi katika jamii akiwaonya watu kuacha kutumia madawa ya kulevya wakati yeye mwenyewe ni mtumiaji.Unaweza kuona wanachokiishi ni tofauti kabisa na wanachakizungumza.kwa daktari alichohitaji ni taarifa ya namna ya kuacha uvutaji na kiongozi ni jinsi ya kuacha madawa.kwa namna nyingine tunaweza kusema wanaishi wasichokikusudia.

 Wote wawili wanaufahamu mpana juu ya madhara ya matumizi ya vitu hivyo  na hata namna ya kuyatibu madhara hayo.Wanachokikosa ni taarifa sahihi ya namna wanavyoweza kuondokana na matumizi ya vitu hivyo haramu.Taarifa nyingi za kujitoa katika uvutaji wa sigara na madawa ya kulevya ziko katika maandishi kila mahali.

Msomaji wa vitabu hubaki halisi kwa namna anavyoishi,maelezo yake na hata mifano anayoitoa.Yote hayo hutokana na kuwa na hifadhi kubwa ya taarifa sahihi alizonazo katika fikra zake. Kwa maelezo mengine ni kusema kuwa, kushindwa kokote ni kutokana na kukosa taarifa za kutosha kuhusiana na kilichoshindikana.

4. KUKUWEZESHA KATIKA KUCHAGUA MTU WA MFANO KATIKA MAISHA YAKO

Mtu wa mfano ni muhimu sana japo si lazima katika maisha ya kila binadamu (role-model).Kwa wengi huyu ndiye amekuwa dira katika mchakato wa kufanikisha malengo maalumu katika maisha.

Japo wanafalsafa wanasema kuwa binadamu anaweza kujifunza ukamilifu kutoka kwa MUNGU ambaye ndiye mfano wa ukamilifu kutokana na ukamilifu alionao.Lakini unaweza kujazwa nguvu zaidi kuufikia ukamilifu huo kupitia wanadamu wenzako wanaopitia njia zile zile unazozipitia wewe.

Kwa msomaji wa mara kwa mara wa vitabu hachukui muda mrefu kukutana na mtu wa mfano kwa maisha yake.Hiyo inatokana na kuwa ,historia za watu muhimu na mambo mengi huwa katika maandishi tena kwa kujirudiarudia. Kwa maana hiyo inakupasa kujenga tabia ya usomaji wa vitabu na maandishi mengine ambayo ndiyo njia rahisi ya kujikusanyia taarifa kwa wakati tunaouhitaji.

5. KUKUPA MAWAZO NA TAARIFA BILA KUKUTANA NA WATU

Kwa namna ya pekee sana unaweza kutumia usomaji wa vitabu na maandishi mengine kupata mawazo mapya na taarifa mbalimbali bila kukutana na mtu yeyote.Kama hutatumia njia hii ya usomaji utalazimika kuwatafuta watu wakupatie taarifa na mawazo mapya kila siku.Ukweli ni kwamba utakuwa umejidhurumu vya kutosha kwa kuwa hutakuwa na uwezo wa kukutana na watu wengi, tena wale unaowahitaji katika maswala muhimu.Vivyohivyo si rahisi kuwafikia wote kutokana na umbali, muda na sababu nyinginezo.

Kitu muhimu unachoweza ni kijifunza mbinu hii inayoyotumiwa kwa karne nyingi sasa kujipatia taarifa na mawazo mapya kila siku.Mbinu hiyo ni usomaji wa vitabu na maandishi mengine .Bila shaka hutapoteza muda tena na utaanza leo kutumia njia hii ya usomaji kujipatia kila aina ya taarifa hapa duniani. kila la heri.


JINSI YA KUJENGA TABIA YA USOMAJI VITABU

Usomaji wa vitabu imekuwa ni nguzo thabiti ya kupata taarifa kwa watu wengi sana .Faida za usomaji wa vitabu  na jinsi ya kusoma kwa kuelewa nakufaulu nimekwisha eleza katika mada husika waweza kubofya link nilizozitaja.Kunachangamoto kubwa inayosumbua  watu wengi nayo ni kukosa  tabia ya usomaji wa vitabu.

Tabia ya usomaji vitabu sio kitu kinachotengenezwa mara moja bali hujengwa kwa muda mrefu kwa kuzingatia hatua kadhaa na baadhi yake ni kama  ifuatavyo.

Kila siku duniani kuna mambo mapya na yanayohitaji ufafanuzi wa kina.Pamoja na kuwepo kwa vyombo vya habari lakini bado jukumu la kujifahamisha kwa kina kuhusu mambo mapya ni lakwako.jenga mazoea ya  kutafuta taarifa za kina kupitia vitabu kwa kila jambo jipya hata kama ni dogo.Kwa kufanya hivyo utapata faida lukiki zitakazo kufanya kila siku kutafuta taarifa mpya na hivyo kua ni tabia yako.

Faida utakazopata ni pamoja na,
      ·         Kuepushwa na upotoshaji au uyumbishwaji  hasa kwa mambo muhimu,
      ·         Kua na ufahamu mkubwa juu ya mambo mengi yanayotakiwa na jamii mfano mambo ya sheria,afya,kilimo,uchumi,biashara,siasa nk,
      ·        Kua kivutio kikubwa kwa watu hasa linapokuja swala la kuelimishana,
      ·     Kujawa na mifano iliyo hai hasa linapofikia swala la kufanya maamuzi magumu.Pamoja na faida nyinginezo.

Kufanya hivyo kuna weza kukukutanisha na mambo mazuri yatakayofanya iwe ni tabia yako.Kama utajenga mazoea ya kusoma kila maandishi yaliyo mbele yako iwe ni kitabuni ,ukutani au mahala pengine popote basi huo ndiyo utakuwa mwanzo wa kujengeka kwa tabia ya usomaji vitabu.Kama hutaweza kusoma hata tangazo lenye maneno 36 tu basi ni vigumu sana kuweza kusoma kitabu chenye maneno  2000 au zaidi.Ni lazima uanze kujenga mazoea ya kusoma vitu vichache na mwishowe itakuwa ndiyo tabia yako ya kila siku.

Kusoma kilichosomwa na wengi kutakusaidia kuanza kujiamini katika usomaji wako na kwa sehemu kubwa ufahamu wako kufanana na kundi la wasomaji wengine.Kitendo hicho kitakufanya kuanza kupata wanachama au kufahamiana na wasomaji wengine wa vitabu watakaozidi kukushawishi kusoma vingine zaidi.Kwa kadiri utakavyo soma na kusoma ndivyo utakavyokuwa na tabia ya kusoma na kusoma.

Kuna watu ambao hawajawahi kufika maktaba kwa miaka mingi sana tangu walipohitimu masomo yao ya ngazi flani. Tena kuna wengine ambao hawajui hata maktaba inafananaje.Mara utakapofika maktaba utakutana na utitiri wa vitabu vyenye mada mbalimbali za kuvutia.Mada nyingine ni zile zenye majibu ya maswali yetu muhimu ambayo tumekua tukiulizana kila kukicha.

Mfano wa mada hizo ni zile zinazohusiana na dunia na mazingira tunayoishi,teknolojia na maendeleo yake,Chanzo cha magonjwa mbalimbali na matibabu yake,Historia za mambo muhimu duniani, uafafanuzi wa mambo mbalimbali ya kisiasa na kidiplomasia,Elimu ya malezi na uongozaji bora wa kifamilia na ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya kisaikolojia.

Kadiri utakavyoendelea kutembelea maktaba ndivyo utakavyozidi kutamani kufahamu mengi kwa kutamanishwa na vichwa vya mada zilizomo kwenye vitabu.Mwishowe utajikuta umejenga tabia ya usomaji wa vitabu.Nashukuru kwa kuwa pamoja nami nakutakia usomaji mwema wa vitabu.