Jumapili, 15 Juni 2014

SABABU ZA KUFELI MTIHANI


Baada ya kutatua tatizo la uandikishwaji  wa wanafunzi wapya mashuleni na vyuoni  kila mwaka, karibu duniani kote,Hivi sasa kumeibuka tatizo jipya la kufeli mitihani.Tatizo hili ambalo wengine kwa kuogopa neno matatizo  wamelibatiza jina changamoto, limekuwa kubwa karibu duniani kote.

Kwa ufupi karibu kila mahali duniani uandikishwaji (udahili) wa wanafunzi wapya umeongezeka.

Mfano mzuri ni kwa Tanzania ambayo ni moja ya nchi ya mfano kusini mwa jangwa la sahara. Ilitimiza dira ya maendeleo ya dunia ya elimu ya mwaka 2025 kwa kufikia uandikishaji wa 103% hapo mwaka 2012.Vile vile takwimu za banki ya dunia zinaonyesha kuwa mpaka kufikia mwaka 2010 ilifikia 95.4% ya uandikishaji wa wanafunzi kwa shule za msingi toka chini ya asilimia 60% mwaka 2000.

TAKWIMU KWA UFUPI

Mafanikio hayo sio kwa Tanzania tu, bali zipo na nchi nyingine zilizofanya vizuri katika uandikishaji wa watoto shule . Miongoni mwa nchi hizo ni

ARMENIA 114 mwaka 2009,    AUSTRALIA 100% mwaka 2009,

BAHAMAS, THE 103% mwaka 2009 ambayo ilishuka 1% mwaka uliofuata,

BANGLADESH 105% mwaka 2009,   GHANA 100% mwaka 2013,

GERMAN 100% mwaka 2009,   CHINA 100% mwaka 2009,

GUYANA 108% mwaka 2009, UNITED STATES 100% mwaka 2009 na kushuka 2% mwaka 2012.

kwa nchi za afrika mashariki

KENYA 98% mwaka 2009 na hakuna takwimu kwa miaka iliyofuata,

UGANDA 102% mwaka 2011,

BURUNDI 99% mwaka 2012,

RWANDA 103% mwaka 2009 na kushuka 1% mwaka 2012.

Takwimu hizi ni kwa mujibu wa bank ya dunia kwa watoto wenye umri wa kwenda shule.
Kutokana na kuongezeka kwa uandikishwaji wa watoto shule za msingi hata sekondari na vyuo vimepata ongezeko kubwa la wanafunzi wapya kila mwaka.Isingetosha kutazama takwimu kwakua sio mada yake.

TATIZO LA KUFELI MITIHANI.

Tatizo hili limekuwa ni kubwa sana na kuwaathili  wazazi ,walezi ,walimu ,serikali na hata  wanafunzi wenyewe.Ukubwa wa tatizo umesababishwa na wadau wenyewe wa elimu ikiwamo wanafunzi.Mbaya zaidi ni kwamba katika kushughulikia hili tumejikita zaidi katika mambo ambayo yako nje ya uwezo wetu na sio yaliyo ndani ya uwezo wetu.

Leo ukimuuliza mtu kwa nini wanafunzi wanafeli mitihani? Atakujibu kirahisi tu kuwa madawati hayatoshi.mwingine atakwambia walimu hawatoshi.
Ninachotaka kusema ni kuwa hata kama kila mtu atakaa kwenye kiti chake darasani na kupata mwalimu wa kumfundisha peke yake, kunauwezekano bado wa kupata watu wanaofeli mitihani. Najua utashangaa kidogo kwa maelezo hayo yaliyo kinyume kabisa na mawazo ya wengi.Ila utanielewa katika kipengele kinachofuata.

KWA NINI WATU WANAFELI MTIHANI

Tatizo kuu la watu kufeli mtihani ni kutoelewa walichojifunza au kuelewa kwa kiasi kidogo sana.Kutoelewa kunatokana na sababu kadhaa ambazo zimeorodheshwa hapo chini tafadhali pitia kwa umakini.

1.UWEZO MDOGO WA KUELEWA HARAKA

Kila mtu hapa duniani ana akili,tena akili za kutosha, isipokuwa kwa wale wenye magonjwa yanayohusiana na akili.Kusema hivyo ni kwamba kila mtu anauwezo wa kufaulu mtihani, ilimradi tu kama alipata nafasi ya kujifunza.

Watu wenye uwezo mdogo wa kuelewa haraka huwa wanafeli kutokana na kutopata muda wa kutosha kueleweshwa.Kundi hili lina idadi kubwa sana ya watu mashuleni kuliko wale wanaoelewa haraka.Kwa kawaida mwalimu hutumia dakika zisizozidi 40 darasani akifundisha.Ni dhahili kuwa muda huu hautoshi kufanya kila kitu kinachomwezesha mwanafunzi kubaki ameelewa 100%.Hivyo kundi la hawa wanafunzi wasioelewa haraka hubaki na pengo la kuelewa kila siku wanapotoka darasani.

Wakati bado wanashughulikia pengo lao ili wafanane na wale wenzao walioelewa,  hujikuta wakikabiliwa na mitihani.Matokeo yake hujikuta wakijibu mtihani ama kwa jinsi wanavyoelewa wao au kwa kubahatisha, hivyo kufeli mtihani.

SULUHISHO.

Ni vizuri kujikagua hasa kwa wale wanafunzi wakubwa, kama unatatizo la kutoelewa haraka.Utafahamu kirahisi kama unatatizo hilo kwa kujipima na wenzako ambao mnajifunza pamoja kwa kuona wakiwa wameelewa na wewe ukiwa bado.Pia unaweza kujipima kwa kujiuliza maswali madogo madogo yanayohusiana na ulichojifunza kuona kama unaweza kujijibu. Pia kwa wale wenye watoto unaweza kumpima  kwa kumlinganisha na watoto wengine au kwa maswali madogo madogo.

Utatuzi sio kwenda ( kumpeleka mtoto)  tuition, kwani hata huko unaweza kukumbana na tatizo lilelile.Cha kufanya ni kutumia muda mrefu zaidi kujifunza kitu kilekile hata kama ni kwa mwalimu yuleyule mpaka uelewe.Hapo ndipo utakapoona unafaulu.kumbuka hata ulipoanza kujifunza kusema  ungali mdogo, ulikosea kila neno ,lakini kila siku ulirudia maneno yaleyale mpaka sasa huhitaji hata kujikumbusha unapotaka kuyatumia.


2. ULEMAVU
Kama mwanafunzi hajakaguliwa sawasawa kuhusiana na ulemavu na kuhudumiwa kipekee ,kunauwezekano mkubwa wa kufeli mtihani.ulemavu ambao una madhara makubwa sana katika ufaulu ni pamoja na ulemavu wa akili,uoni hafifu na kutosikia vizuri.Kuna baadhi ya wanafunzi wenye uoni hafifu au kutosikia vizuri wasiojulikana na walimu wao.Kwasababu ya kutojulikana kwao hujikuta wakijifunza kwa mashaka tu mpaka mwalimu  anamaliza kufundisha  darasani.Matokeo yake hujikuta wakiwa hawajaelewa mpaka mitihani inapowakuta.

SULUHISHO

Ni vema kujikagua au kumkagua mwanafunzi kama ana matatizo niliyokwisha yataja.Endapo kama unamatatizo hayo au mojawapo basi ni vema kuhakiki kuwa hayaathili kuelewa kwako.Kama yana athili basi tumia njia inayokufanya uelewe na sio kubaki na deni la kutoelewa kila utokapo darasani.

3.UWEZO MDOGO WA KUCHUKULIANA NA MAZINGIRA

Mwanafunzi mwenye uwezo mdogo wa kuchukuliana na mazingira, anaweza kuelewa taratibu au kutoelewa kabisa na kujikuta akifanya vibaya katika mitihani yake.Hapa ndipo unapokuja ule usemi ninaoupenda sana usemao kile usichoweza kukizuia kiepuke.

Mazingira yanaweza  kumuathili mwanafunzi endapo kama hatoelewa nini cha kufanya wakati yanapofikia hatua ya kuathili uelewa wake darasani.
Hapa ndipo unapoweza kuona tofauti .Kwamba mwanafunzi anayeishi katika mazingira magumu au kutoka familia yenye kipato kidogo na vyenzo chache za kujifunzia anafaulu mtihani, lakini Yule mwenye kila kitu anafeli.Yote inatokana na uwezo wa kifikra alionao mwanafunzi katika kukabiliana na mazingira kama hayo.Uwezo huu huwa ni wa kibinafsi zaidi na sio ule unaotokana na mafunzo maalumu.


Mazingira yenye athali yanaweza kuwa uchumi duni,uhaba wa walimu au wakufunzi,umbali wa shule au chuo,uwezo mdogo wa walimu au wakufunzi kufundisha,nyenzo chache za kujifunzia au  kufanya mazoezi (practicals),changamoto za kirika (mapenzi,starehe).Hivi vyote ni vikwazo katika kuelewa kwa mwanafunzi shuleni.

SULUHISHO

Kama kunamazingira yeyote yanayokufanya au yanayomfanya mwanafunzi kushindwa kuelewa darasani au kwingineko, jambo la kwanza ni kuyaepuka.Ikiwa ni umbali tafuta kukaa karibu na shule/ chuo,kama ni uwezo  duni wa walimu au wakufunzi tafuta wakufunzi,kama ni nyenzo chache jifunze kutumia zilizopo au zinazopatikana kwingineko.

Tafuta na kuelewa kama udhaifu  wa kuelewa kwako  darasani  unasababishwa na mazingira uliyonayo. mazingira usiyoweza kuyakabili unachofanya ni kuyaepuka .Kuepuka ni njia rahisi sana katika mapambano yeyote yale.Nafikiri endapo kama utapewa miujiza ya kuweza kukwepa masumbwi yoyote hapa duniani, basi ungelijitosa katika mashindano ya masumbwi ya pesa nyingi kwa kutegemea uwezo wako wa kukwepa masumbwi.Ungefanya hivyo kwa kuwa usingetegemea kupangua au kuhimili kipigo cha konde lolote kutoka kwa mshindani wako kwa kuwa unauwezo wa ajabu wa kukwepa makonde.

Endapo mazingira uliyonayo hayaepukiki basi njia ya pili ni kujenga nayo urafiki ili uyatumie kwa manufaa yako.Anza kujenga ukakamavu wa kuishi katika mazingira ambayo huyapendi ili yasiharibu uelewa wako darasani.

Sote tunafahamu kuwa gerezani ni mahala penye maisha magumu sana ,lakini mfungwa anaweza kuishi miaka 30 na zaidi.

Sote tukisikia mlipuko wa bomu au risasi tunakimbia hovyo ,lakini askari anaweza kukaa vitani na milipuko hiyo mpaka atakapopata amri ya mkuu wake kuondoka ili asifukuzwe jeshini.

Sote tunafahamu kuwa ni vigumu kwa binadamu yeyote kukaa macho usiku mzima bila kulala, lakini leo tuna mamilioni ya watu duniani wanaokesha kwa hiari yao viwandani ili mwisho wa mwezi waweze kujipatia kipato.

Kwasababu hiyo hata wewe unaweza kujenga ukakamavu wa hiari kukabiliana na mazingira uliyonayo ili yasipunguze uelewa wako darasani .Kwa kuzingatia ushauri huu nina imani sasa hautafeli tena mtihani na utakuwa msaada kwa wengine.


Usikose ku “ LIKE” page yetu ya facebook ujipatie masasisho mapya kila yanaporushwa kwenye mtandao. karibu. https://www.facebook.com/pages/Free-tuition/260313704137723?ref_type=bookmark

Maoni 1 :

  1. Ni kweli unachokisema ila mwanafunzi hasa kwa umri wake huwa ni vigumu kutilia mkazo mambo ya msingi ikiwa hakusimamiwa na kufuatiliwa ipasavyo na mzazi au mlezi wake.Mzazi au mlezi mwenye uwezo wa kufanya kazi hii ni yule ambaye ana ufahamu juu ya anachokifuatilia. Ungana nasi AMIP-TANZANIA tukatoe elimu kwa wazazi hawa watimize majukumu yao ipasavyo.

    JibuFuta