Jumanne, 27 Mei 2014

MBINU ZA KUSHIDA DHANA POTOFU ZA ELIMU

Lengo la mada hii ni kutaka kukukumbusha kuwa kuna dhana potofu zinazo husu elimu.Dhana hizo ambazo naziita potofu kwa kuwa zimekuwa hazina uhalisia wowote zaidi ya kurudisha nyuma maendeleo ya wasomi wetu.Dhana potofu ni fundisho linalodhaniwa kuwa ni kweli wakati si kweli au ni uongo unaodhaniwa kuwa kweli hivyo kuaminiwa na wengi.Miongoni mwa dhana hizo ni kama ifuatavyo:-
     1 .     ELIMU HAINA MSAADA WOWOTE  BILA PESA

kumekuwa na dhana hii kwa muda mrefu sasa.Imewafanya watu wengi hata wale walio masomoni wakati mwingine kuachana na masomo na kukimbilia kutafuta pesa ndipo warudi kutafuta elimu.

 Sina maana kuwa kama unasoma huwezi kutafuta pesa, bali natilia mkazo kuiondoa dhana hii ili wale walio katika mazingira ambayo hawawezi kufanya vyote, wajitahidi kumaliza madaraja yao ya elimu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kiutafutaji.

Dhana hii haina ukweli wowote na hutumiwa na watu wasiopenda elimu kwa kupenda njia fupi na za mkato.kupitia elimu ndipo tunapokuwa na mipango mizuri ya upataji pesa.Elimu hii kama hatukuipata darasani tutalazimika kuitafuta nje ya darasa.Endapo tutakuwa na elimu tena elimu ya kutosha kuhusiana na jambo lolote lile ,ndipo tutakapokuwa na fursa za kutosha katika kutafuta pesa.

MFANO,Mfanya biashara msomi endapo atapoteza biashara yake katika mazingira ya aina yeyote, bado atakuwa na nafasi kubwa ya kupata ufumbuzi wa tatizo lake kupitia elimu aliyonayo.Kupitia elimu aliyonayo atakuwa na nafasi ya kushindana katika soko la ajira na kupata kazi ya kufanya itakayompatia mtaji mpya.Pia ananafasi kubwa ya kuendeleza biashara yake kwa kuwa na nyenzo za kutosha kukuza biashara.Nyenzo hizo ni pamoja na-

·         Anajua kusoma na kuandika hivyo atatumia fursa hiyo kuratibu biashara yake kwa kuhifadhi
kumbukumbu,kusoma vipeperushi na majarida kwa ajili ya kupata taarifa muhimu za biashara inayomuhusu.
·         Ataadika mchanganuo wa biashara kwaajili ya kupata mikopo kwenye taasisi  za fedha  tofauti na mtu asiye na elimu ambaye atalazimika kuitafuta  elimu hiyo wakati huo.
·         Endapo biashara itakuwa kubwa bado atakuwa na fursa ya kuisimamia kwa kuwa anao ujuzi wa kusimamia biashara na kufanya shughuli za kiofisi.
kivyovyote vile kazi anazoweza kufanya mtu asiye soma mtu yeyote aliyesoma anaweza kufanya .Lakini cha kusikitisha ni kwamba sio kazi zote anazoweza kufanya mtu aliyesoma asiyesoma anaweza kufanya .Hapo unaweza kuona jinsi mtu aliye na elimu anavyokuwa na wigo mpana katika kutafuta mafanikio bila hata kuwa na pesa.



      2 .       KUFANIKIWA SIO LAZIMA UWE NA ELIMU
Ikumbukwe kuwa watu wote waliofanikiwa wametumia elimu. kama hawakuitumia rasmi basi waliitumia bila wao kufahamu.Kitu kisicho fahamika ni kuwa hawakutumia elimu rasmi katika kufanikiwa kwao kutokana na sababu mbalimbali.

*Wapo wasiotumia elimu hiyo rasmi kwa kuwa hawakuwa na uwezo wa kuifikia.
*Wapo waliokataa kwa makusudi kwa kudhani kuwa kusoma kwanza ni kupoteza muda.
*Wapo walioikosa kutokana na sababu za kukatishwa kutokana na maswala yaliyokuwa nje ya uwezo wao na sababu nyinginezo.


Kwa wale waliofanikiwa bila kupata elimu ,Kuna uwezekano mkubwa kuwa walitumia nguvu nyingi sana kuliko mafanikio waliyoyapata. Sababu  kubwa  ni kuwa walifanya vyote kwa wakati mmoja yaani kutafuta elimu huku wakitafuta mafanikio.Kwasababu hiyo kwa mtu anayetaka mafanikio yatakayoendana na kiasi cha nguvu anayowekeza ni lazima akubali kujielimisha kwanza.


      3.       UNAWEZA UKASOMA  NA USIPATE KAZI
Hii nayo ni dhana potofu .Imetumiwa na watu wengi katika kujifariji na kutochangamkia fursa za elimu kwa kuogopa kuwa watapoteza muda wao kusoma kisha wasipate kazi.Watu wenye mitazamo ya namna hii mara nyingi wamefikiri zaidi kuajiriwa kuliko kutengeneza ajira .
Mtu mwenye elimu kama ataitumia elimu yake sawasawa anaweza kutengeneza ajira yake binafsi na baadaye kupitia ajira yake akazalisha na za wengine.

mfano muhitimu wa daraja la diploma wa chuo cha hoteli badala ya kuzunguka mwaka mzima akitafuta kazi ya umeneja mahotelini na kuambulia mshahara kiduchu.Anaweza kutumia elimu aliyoipata kufungua mgahawa wake mitaa ya nyumbani kwake na kutengeneza vyakula asili vya watu waliomzunguka .kwa kutumia ujuzi mkubwa alionao ni wazi kuwa huduma zake zitakuwa bora kuliko wale wote wanaofanya shughuli hizo bila elimu, hivyo kuvuta wateja wote kwake.Ni dhahili kuwa baada ya miaka michache asizungumze tena kuhusu kuandaa vyakula bali kumiliki mgahawa wa kisasa kama si hoteli.

Pia hata kwa wahitimu wengine wanaweza kuanzisha ajira zao wenyewe kupitia wao binafsi au vikundi kulingana na taaluma husika. Hivyo si kweli kwamba kuna mtu anaweza akasoma na asipate cha kufanya.



      4.       UKISOMA SANA HUTAPATA AJIRA KWA KUWA WAAJIRI WATAOGOPA KUKUAJIRI
Dhana hii nayo siyo sahii japo hata baadhi ya wasomi wamekuwa wakiitumia.Kinachotakiwa ni kufikiri zaidi jinsi utakavyoitumia elimu kubwa utakayokuwa nayo na si jinsi watu wengine watakavyoitumia elimu kubwa uliyonayo.

Uwoga huu ndiyo unaoleta dhana hizi potofu na kuzifanya ziwe na nguvu katika jamii.Elimu ya kiwango cha juu ndiyo inayohitajika katika dunia.Mtu mwenye kiwango kikubwa cha elimu si bidhaa tu kwake na kwa  kwa wanaomzunguka bali ni bidhaa pia katika ulimwengu .Elimu kubwa inahitajika kwa mtu binafsi,kwa jamii inayomzunguka na hata kwa ulimwengu mzima.

Sote ni mashahidi wa mageuzi makubwa yanayofanyika ulimwenguni.Iwe ni mageuzi ya kiteknolojia ,kiuchumi,kielimu,kitabibu,nk mengi yamefanywa na watu waliobobea katika elimu husika.

Sina maana kuwa watu wasio na elimu kubwa hawana mchango katika maendeleo,bali walio na elimu ya kati wakisaidiwa na wenye kiwango cha juu cha elimu ukijumlisha na vipaji walivyonavyo wanafanya maajabu zaidi.

fikiri kuwa elimu vyuoni ingekuwaje kama kusinge kuwa na watu waliobobea kufundisha,mahospitalini matibabu yangekuwaje kama kusingekuwa na mabingwa,katika biashara na uchumi, sote ni mashahidi juu ya mitikisiko ya uchumi duniani kuwa  tulihitaji watu waliobobea kiuchumi.
Bila shaka iwe ni kwa matumizi binafsi au ya umma, kusoma sana ni muhimu kwaajili ya maendeleo.

      5.       WASOMI WA ZAMANI NDIYO BORA KULIKO WA SASA
Kuna wanaodai kuwa wasomi wa zamani ni bora kuliko wasomi wa sasa hivyo kisomo cha sasa hakina tija.Dhana hii imezungumzwa hata na baadhi ya watu wanaoheshimika katika jamii.Kwa kiasi kikubwa umma umepotoshwa na dhana hizi potofu kiasi cha kutowapa umuhimu wasomi wetu wa sasa kwa kigezo kuwa hawana lolote.

Wasomi ninaowazungumzia hapa ni wa aina zote wawe wale wa kiwango cha shule za msingi au chuo kikuu.Kwa mujibu wa dhana hii wameonekana kuwa hawana lolote na kwa sababu hiyo wale wahitimu wa zamani ndiyo walio bora.Na wengine hasa hapa kwetu tz wamedai kuwa mwanafunzi wa darasa la saba wa mwaka 76 ni bora kuliko Yule wa kidato cha nne cha sasa katika miaka hii ya 2000.

Kunakitu ambacho tunakisahau na ndiyo maana dhana hii inapata nguvu kiasi.Tunachotakiwa kufahamu wakati  tunapofanya malinganisho ya wahitimu hawa tunatakiwa kuangalia vigezo vifuatavyo.
1.       Umri wa wahitimu wa sasa na wale wa miaka ya nyuma
2.       Mitaala ya sasa na ile ya zamani
3.       Fursa za sasa na zile za miaka ya nyuma

UMRI
tukianza na hilo la umri ni wazi kuwa wahitimu wengi wa sasa kwa ngazi yeyote ile wanaumri mdogo kuliko ule wa wale wa miaka ya nyuma.Mfano miaka ya nyuma kwa hapa kwetu Tanzania mwanafunzi wa darasa la saba alikuwa na umri mkubwa kiasi cha kufikia hata 20.Lakini kwa wanafunzi wa sasa wengi wao wana umri wa miaka 14 na 15.

kwasababu hiyo wanafunzi wa sasa wanauwezo mkubwa kifikra kuliko wale wa miaka ya nyuma .Kwasababu mtoto wa sasa wa miaka13 na 14 anauwezo wa kujifunza na kushika mambo ambayo wakati huo yalikuwa yakisomwa na mwanafunzi wa miaka 18 na 20.
Lisha ya hapo wanafunzi wa sasa waanajifunza mambo mengi na Wakihitimu Wanatija kubwa  kuliko wale wa miaka ya nyuma .Ukichukua mwanafunzi wa kidato cha nne wa miaka ya sasa ambaye wastani wa umri wake ni sawa na Yule wa darasa la saba wa miaka ya nyuma yaani miaka 18  mara anapohitimu ,kulingana na mtaala uliopo anafahamu mambo yafuatayo

1. Anafahamu kuhusu mambo yote yanayohusu mwili wake ikiwamo mifumo yote muhimu ikwamo ya uzazi na jinsi ya kujikinga na baadhi ya magojwa.
2.Anafahamu kwa sehemu kubwa mgawanyiko wa wanyama na tabia zao pamoja na mimea na makundi yake na sifa zake.
3 . Anafahamu kuandika barua mbalimbali za kiofisi ikiwamo za kuomba kazi na kuandaa ripoti.
4.Anafahamu kemikali mbalimbali zenye manufaa na zile zisizo na manufaa
5.Anafahamu uandishi wa insha na muhutasari wa maswala mbali mabali ya kijamii.
6. Anafahamu kwa sehemu kubwa utunzaji wa kumbukumbu
7.Anafahamu kwa sehemu kubwa nguvu za asili zilizopo duniani na jinsi zinavyoweza kupimwa.
8. Anafahamu tabia nchi na mambo yote yanayohusiana na tabia nchi ikiwamo hali ya hewa na vipimo vinavyotumika kipimia.
9.Anafahamu historia ya nchi yake na Afrika, madhara ya ukoloni na faida zake,madhara ya kutokuwa na umoja nk.
10.Unafahamu maswala muhimu ya uraia pamoja na haki na wajibu wa raia.
11.Anafahamu mifumo kadhaa ya kisasa ya mashine na jinsi inavyofanya kazi.
12.Anaelimu ya mauzo na manunuzi
13.Anafahamu matumizi ya komputa na faida zake
14.kama ni mwanafunzi wa shule za ufundi ana jua uselemala,ujenzi,upauaji,na mambo mengine ya ufundi.


Muhitimu huyu kama nitaamua kuandika habari zake zote ni wazi kuwa ukurasa huu hautatosha.kwa ushahidi huu naweza kusema kuwa muhitimu huyu wa sasa anatija kubwa kwa kuwa katika umri mdogo tayari anafahamu vitu vingi.

Mifano ya ushahidi wa manufaa hayo ni wamefanya vizuri katika majeshi yote,viwandani,katika biashara ndogo na kati,katika kilimo nk.
MTAALA
Mtaala wa zamani ulilenga kumwandaa mwanafunzi kuishi katika ujamaa na kutumia rasilimali zilizomzunguka.Lakini mtaala wa sasa unalenga kumwandaa mwanafunzi  kuendelea na elimu inayofuata vilevile kuingia katika soko la ajira.Mpaka hapa utaona jinsi mwanafunzi wa sasa alivyo na tija zaidi.

FURSA.
Hili ndilo swala linalosababisha wahitimu wa sasa waonekane hawana lolote .Wahitimu hao ni pamoja nawale wa vyuo vikuu.Wahitimu wa sasa wanachokikosa ni fursa.Wengi wao wanaonekana hawana lolote kwasababu ya kukosa cha kufanya.Wakati wa miaka ya nyuma wahitimu wote waliingizwa kazini kinyume na wahitimu wa sasa ambao baada ya kumaliza masomo yao wamejikuta wakigonga ukuta katika soko la ajira.Takwimu zilitolewa hivi karibuni na BARAZA LA VYUO VIKUU AFRIKA MASHARIKI  zinaonyesha kuwa  nchini Tanzania ni 38% tu ya wahitimu wa vyuo ndiyo wanaopata ajira baada ya kuhitimu masomo yao.

 Aidha kwa mujibu wa takwimu za wizara ya kazi na ajira za mwaka 2006 kupitia utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi ulibaini kuwa,jumla ya wahitimu wa stashahada 1.160 kati ya wahitimu 35,875 hawakuwa na ajira na jumla ya wahitimu 3,092 kati ya 45,600 wa shahada na stashahada za juu hawakuwa na ajira nchini Tanzania.

kwasababu hiyo kilichopo ni kuwaimarisha wahitimu waweze kujiamini na kutengeneza ajira binafsi.







       6.       ELIMU NI GHARAMA SANA HIVYO WENYE PESA NDIYO WANAOMUDU
Kifupi naweza kusema kuwa elimu ni gharama kama utahitaji elimu ya namna hiyo.Kwa mtu anayehitaji elimu kwa gharama ndogo anaweza kuipata.Kwa mtafuta elimu atatumia njia zote za kutafuta elimu ikiwamo maktaba ambazo zimekuwa zikitoa fursa ya watu kupata elimu kwa gharama inayoweza kumfanya kila mtu kumudu.

      7.       SIO VIZURI KUSOMA VITU VINGI
kifupi naweza kusema kuwa hakuna utafiti wowote wa kisayansi uliopendekeza kuwa kusoma vitu vingi kunamadhara .Utafiti umeonyesha kuwa ubongo wa mwanadamu unauwezo wa kuhifadhi kumbukumbu zote tangu kuumbwa kwa mwanadamu hata dunia itakapoisha  na bado kukawa na nafasi katika ubongo.Utafiti uliofanywa umeonyesha kuwa ubongo unahifadhi kumbukumbu taratibu sana ,Hivyo hakuna hofu kuwa ukijifunza vitu vingi eti sio sawa.

kulingana na mchango huu hata kama hautakidhi kikamilifu kukuondoa kwenye dhana potofu zinazohusu elimu bali utakuwa umenufaika katika maeneo machache niliyoyagusia japo nimefanya hivyo kwa kifupi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni