Jumatano, 21 Mei 2014

JINSI YA KUFAULISHA MITIHANI KIDATO CHA NNE TANZANIA



Hivi sasa Tanzania kumekuwa na mfurulizo wa kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa kasi kubwa.Shwala hili limeleta mvutano na malalamiko mengi miongoni mwa jamii hususani wapenda elimu.

Malalamiko yaliyojitokeza kufuatia kushuka kwa kiwango cha ufaulu ni kama ifuatavyo:-

1.Serikali imeshindwa kuboresha mazingira ya elimu yaani hakuna ,shule za kutosha,vitabu,maabara,walimu,waliopo wengi wao wamepata mafunzo ya muda mfupi,kiwango cha ufaulu cha wanao kwenda kusoma ualimu ni cha chini mno, mishahara midogo,kutelekezwa kwa shule za kata, mengine ni:-

masomo ni mengi kupita uwezo wa uelewa wa wanafunzi,matumizi ya lugha ya kigeni kufundishia,mfumo mbovu wa elimu yaani kubadilika badilika kwa mtaala, nk.

2.Walimu wamelalamikiwa kwa kujali zaidi shughuli binafsi kama tuition na kadhalika kuliko kufundisha darasani.

3. Wasimamizi wa elimu hawaja chukua majukumu yao ya msingi kusimamia elimu ipasavyo, nk.

4.ukosefu wa nyumba za walimu na mabweni kwa wanafunzi wa kike.

Pia kumekuwa na malalamiko mengine mengi ambayo serikali inalaumiwa ambayo nisingeweza kuyataja kutokana na uwingi wake.

MASWALI YA KUJIULIZA KABLA YA KULAUMU

1.Kama kiwango cha elimu kimeshuka kutokana na upungufu wa shule je ni lini huko nyuma shule zilitosha na kutapakaa kila mtaa na ndiyo ikawa sababu ya ufaulu mkubwa?.

2.Ni lini siku za nyuma vitabu,maabara,na vifaa vingine vya kufundishia vilitosha na ndiyo maana tulikuwa na ufaulu mkubwa?

3.Ni lini waalimu walitosha siku za nyuma ndiyo maana tulikuwa na ufaulu mkubwa?

4.Ni wakati gani siku za nyuma serikali ilikuwa ikipeleka wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza kusomea ualimu na ndiyo sababu tukawa na ufaulu mkubwa?

5.Kuhusu mafunzo ya muda mrefu je! Hatukuwahi kuwa na walimu wa UPE na wakafanya vizuri siku za nyuma?

6.Kuhusu kubadilika kwa mitaala, je ! kuna umuhimu wowote kuendelea kubaki na vitu ambavyo vimekwishapitwa na wakati katika mitaala ili kuzalisha division one?

7.Kuhusu matumizi ya lugha ya kigeni ,je! kunawakati tuliwahi kutumia Kiswahili kufundishia siku za nyuma? Katika somo la Kiswahili utafiti umeonyesha kuwa watoto wote hupata daraja la kwanza?

8.Kuhusu mishahara ,inamaana wale walimu wa zamani walikuwa wakilipwa kwa masaa kama ilivyo kwa baadhi ya maprofesa wanaofundisha vyuo zaidi ya kimoja?

Ni wazi kuwa kila swali jibu lake ni HAPANA. Hiyo inaonyesha kuwa kuna kitu tunacho kisahau wakati wa kufanya majumuisho nani wa kumlaumu na nini tufanye kuokoa ufaulu wa watoto wetu.

NINI CHA KUFANYA KUONGEZA UFAULU


Tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu sababu za kushuka kiwango cha ufaulu zililenga taasisi za elimu. Tafiti hizi ni pamoja na zile za serikali yenyewe na hata za taasisi za kiraia kama TWAWEZA nk.Vile vile tafiti hizo nyingi mapendekezo yake yahusisha gharama kwa serikali.

Lakini swala la kuanguka kwa ufaulu ni zaidi ya taasisi za serikali. Kuna uwezekano wa kuleta mabadiliko bila ya kutumia gharama kubwa kama tunavyodhani .Hili tumeliona kupitia mitazamo ya watu wengi hata kwa baadhi ya viongozi wa serikali kama wabunge na wengineo.Wengi wamekuwa wakilalamikia bajeti ndogo ya elimu inafanya kiwango cha ufaulu kushuka bila kujua kuwa huko nyuma tulikuwa na bajeti ndogo kuliko hizi za sasa.

katika swala hili kila mtu anachangia kwa namna yake ikiwamo mimi na wewe.Na kama kweli tukiamua kukomesha tatizo hili tuna uwezo wa kubadili matokeo ndani ya mwaka mmoja.Ila kama tutaendelea kumtafuta mchawi basi mpaka masihi atakaporudi bado atakuta tuna mtafuta mchawi na hatutampata.

Kuna hatua za ujumla za kuchukua ili kunusuru janga hili na wala hazihitaji gharama ya ziada nazo ni kama ifuatavyo:-

1.KUDHIBITI VYETI FEKI


Hili ni swala linalomuhusu kila mtu.vyeti feki ni vile vyeti vinavyotumiwa na baadhi ya walimu wanafunzi katika kujipatia fursa ya kusoma ualimu bila kuwa na sifa halali.Hawa ni watu wenye shida ya ajira lakini hawana lengo la kufundisha watoto.Wamekuwapo shuleni kutimiza idadi lakini mchango wao hauna tija hata kidogo.mimi na wewe tukikataa kuwapa vyeti vyetu au kuwatengenezea vyeti feki basi hakutakuwa na walimu wa namna hii.
Serikali kwa upande wake iwa badilishe wale walioingia kwa vyeti feki kwa kuwaweka wale halali.

2.WALIMU WALIOPO WAFUNDISHE.

Bila kujali uchache wao au kuchelewa kwa posho walimu waliopo wafundishe.Hata kama shule inamwalimu mmoja anatakiwa afundishe.kwa kufanya hivyo atakuwa ametimiza jukumu lake la msingi. Wale wanafunzi waliopata nafasi ya kuhudhuria shule siku hiyo watakuwa wamejifunza.Wanafunzi wanachokitaka sio uwingi wa walimu bali ni ubora na uwingi wa topic.


Kitendo cha walimu wa sasa kutumia kisingizio cha kuchelewa kwa posho ,malipo ya uhamisho nk.kutofundisha hakina mashiko.Hapo awali kulikuwa na usumbufu zaidi ya huo lakini bado ufaulu ulikuwa unaridhisha.Walimu wote walikuwa wakilipwa fedha zao mkononi na wengine walikuwa wakifuata mshahara zaidi ya kilometa mia tano safari ya masaa nane kwa basi.Lakini katika kipindi hicho chote bado kulikuwa na ufaulu unaoridhisha.vipi kuhusu hawa wa kidigitali wakibofya tu wanazoa ufaulu kwa nini hauvunji chati?

3.VITABU VILIVYOPO VITUMIKE

Kumekuwa na kawaida ya kufungia vitabu stoo kwa baadhi ya shule na kuwaacha wanafunzi wakiwa wanasoma bila kitabu kwa lengo la kuvihifadhi.Tunachotakiwa kufanya ni kuwapatia wanafunzi vitabu vilivyopo na kuwasimamia kuhakikisha kuwa wanavitumia kwa manufaa.Siku za nyuma kitabu kimoja kilitumika hata kwa watoto sita na ufaulu bado ulikuwa juu.


Wapo waliosoma mpaka wanamaliza hawakuwahi kuona baadhi ya vitabu na walifaulu.Kinachotakiwa sio utitiri wa vitabu bali ni vilivyopo vinatumikaje.


4.TUTUMIE MAABARA ZILIZOPO

Ili mwanafunzi aweze kuelewa sio lazima alale maabara.Anahitaji majaribio machache tu kulingana na topic anayosoma.Na wala sio majaribio yote yanahitaji maabara, mfano kujua mfumo wa uzazi wa panya sio lazima jaribio lifanyikie maabara, bali vifaa vichache tu vinavyoweza kuandaliwa hata na mwanafunzi mmoja tu na jaribio likafanyika.

Pia tunaweza kutumia mfumo shirikishi wa maabara.ZOEZI hili ni rahisi sana hasa kwa shule za umma.Shule zinaweza kuanzisha mfumo wa kushirikiana katika kutumia maabara moja wakati wakisubiri zakwao kujengwa.

Maabara moja inaweza kutumiwa na shule hata tano kwa kwa mfumo wa matumizi shirikishi.Kama shule zimeweza kushirikiana katika mashindano ya shule za sekondari ,NA majaribio ya mitihani mbalimbali kwanini zisiweze kwa mambo ya msingi kama haya ya maabara?.

5.TUACHE KUELEKEZA MACHO KUJENGA MASHULE TUU.

Huu upepo wa wazazi kuelekeza macho kwenye kujenga mashule bila kushiriki katika swala la ufaulu linachangia kushusha ufaulu.

Nguvu hii tuliyoitumia katika kujenga mashule tuitumie katika kuinua kiwango cha ufaulu.Wanajamii tunaweza kuanzisha na kudhamini MASHINDANO ya TAALUMA ya KIKANDA kwa SHULE za SEKONDARI ya kila baada ya miezi sita ambapo watoto hamsini wa kwanza wanazawadiwa vifaa muhimu vya shule.ambayo tunaweza kuyaita( MATAKISHUSE).


Hapa tunakuwa tumepiga ndege wawili kwa jiwe moja ,kwanza tutakuwa tumewapa watoto mwamko wa kufanya vizuri ili washinde,tutakuwa tumewawezesha kupata mahitaji muhimu ya shule,wazazi watasimamia watoto wao ili washinde ili wanufaike na zawadi.Na hili linawezekana kama ilivyowezekana kudhamini michezo ya wazee wazima ya kila mwaka kama ya mashindano ya michezo ya vyombo vya habari nk.

Wazazi baada ya kujenga mashule mengi sasa imefika wakati wa kuamua watoto wetu wasome kwa raha bila karaha.

Mfano Badala ya kuendelea kuchangia kila siku swala moja la madawati na matokeo yake dawati moja linakwenda kununuliwa na wajanja wachache hata kwa shilingi milioni moja, sasa tuchangie dawati na si fedha.Kama inakuwa ngumu kwa mzazi mmoja kuchangia dawati moja basi wazazi wawili wanaweza kuchangia dawati moja.Na hili linawezekana kwa kuwa rasilimali zote za kutengenezea madawati tunazo ikiwamo mafundi.

6.TUREJESHE MAADILI

Kama kuna kitu ambacho kimefanikiwa kuua elimu kwa kiasi kikubwa basi maadili naweza kuyapa nafasi ya kwanza.Hakuna mtu anaye hitaji kufundishwa maadili na hakuna mtu anayeweza kusomea maadili na akafuzu. Maadili ni tabia na tabia hufundishwa kwa kuambukizwa na anayeambukiza tabia lazima awe nayo.

Tuwaambukize watoto maadili mema.Hili ni kwa kila mtu kuanzia mzazi,mpitanjia hata kwa mwalimu.Kama mwanafunzi akiwa na maadili akiambiwa sikiliza atasikiliza,akiambiwa andika ataandika,akiambiwa kesho mapema atafika mapema nk.

Tuache kuwaalika wanafunzi katika kumbi za starehe,tusishirikiane nao tunapowaona katika mazingira kama hayo,tuwaelekeze kuheshimu wakubwa kwa kuanza kuwaheshimu wao,tufuatilie mahudhurio yao hata kama hawatuhusu kwasababu hao ndio Tanzania yenyewe.Wakifanya vibaya tunadhalilika wote.

7.WAZAZI WAWAJIBIKE

Wazazi wasiachie shule kila kitu.Mtu wa kwanza kutoa elimu kwa mtoto ni mzazi.Mzazi anafundisha kula,kuvaa,kusalimia,usafi,nk.Lakini linapofika swala la kusoma na kuandika anajitoa, hii si sawa.

Mzazi anawajibu zaidi ya mwalimu kuhakikisha kuwa mtoto anajua kusoma na kuandika na hata kufikia kikomo cha upeo wa mzazi husika.

Maendeleo ya uelewa wa mtoto yanaweza kupimwa zaidi na mzazi kwa kuwa yeye ndiye anayejua hata sababu ndogondogo zinazomfanya mtoto kutokufanya vizuri shuleni.

8.TUWASAIDIE WANAFUNZI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA ELIMU

Wanafunzi wa sasa wanakabiliana na changamoto nyingi sana tofauti na wale wa zamani.
KUTOKANA NA MAENDELEO YA KIUCHUMI watoto wa sasa wanapendeza kimuonekano na kusababisha mizee mizima kuwamezea mate.kwa sababu hiyo wanarubuniwa na kutumia nguvu nyingi kuzingatia masomo.Tuingilie kati mara tunapoona wanapotoshwa na kushawishiwa kukiuka miiko ya wanafunzi.

9.TUWAFUNDISHE KUTUMIA TEKNOLOGIA KIMANUFAA

Siosawa kuwazuia watoto hawa kutumia simu wala computer wakati ndivyo vifaa vinavyotumika katika zama zao kurahisisha shughuli za kila siku.
Chakusikitisha ni kwamba wakati unawazuia wao wanatumia kwa siri.Matokeo yake wanatumia isivyosahihi kwa kuwa hawajui kuwa kunauwezekano wa kunufaika na vifaa hivyo vya teknologia ya sasa.

Kitu cha msingi tuwafundishe wanafunzi wetu matumizi sahihi ya teknologia hizi za sasa na namna wanavyoweza kunufaika nazo kwa kuongeza ufaulu wao.

MATUMIZI YA INTERNET

Mfano ,kupitia simu au laptop mwanafunzi anaweza kudownload notes kwenye mtandao au kutoka kwenye faili la kimtandao la mwalimu wake na kujisomea au kushare na wanafunzi wenzake. Atajuaje haya kama hakufundishwa?

Wanafunzi wanaweza kuanzisha blog yao , website au group lao katika mitandao ya kijamii na kushirikiana katika mijadala ya elimu na kubadilishana notes pamoja na mswali kwa mazoezi.Je wasipoelekezwa kutumia fursa hizi watajuaje?

Kama wanafunzi wakielimishwa zaidi wanaweza kutumia simu zao hata darasani kwa usimamizi maalumu kujifunza baadhi ya vitu ambavyo sio rahisi kupatikana katika mazingira yao.kupitia mtandao wa internet vitu ambavyo wanafunzi wanaweza kujifunza ni pamoja na,

1. Uhalisia wa sasa wa sayari wanayoishi katika picha za hivi karibuni bila kusubiri vitabu vibadilishwe.

2. Mabadiliko mapya ya kisayansi ambayo bado hayajaingizwa kwenye vitabu

3. Mazingira halisi ya maeneo ambayo wamejifunza bila kufika kwa kutazama video zake katika mtandao au simulizi za picha zake.

4. Shughuli mbalimbali za kiutafiti,takwimu,hotuba za viongozi ,historia za nchi mbali mbali nk.

5. Ufafanuzi wa ziada wa baadhi ya topic ambao haumo kwenye vitabu.

6. Taarifa zinazobadilika badilika kama za viongozi wakuu wa nchi na taasisi zake zinazowekwa katika mtandao na mengine mengi.

7. kutumi website zilizo na baadhi ya notes wanazozihitaji kujisomea na kuongeza ufaulu.

8. Kutumia kamusi za kimtandao kupata ufafanuzi wa maswala ambayo hayapo kwanye kamusi zilizo chapishwa au vitabuni.

10.MWANAFUNZI AFANYE WAJIBU WAKE

Wajibu mkubwa wa mwanafunzi ni kusoma na si vinginevyo.kama elimu yake inapatikana shuleni basi apatikane shuleni na asionekane maeneo mengine baada ya muda wa shule.mwanafunzi awe na uchaguzi wa mambo ya kushirika na si kila jambo.


Japo kuna mambo mengine ambayo mwanafunzi anaweza kufanya huku akisoma lakini si yote yanaurafiki na elimu.Ni wajibu wa mwanafunzi kuchagua masuala ya ziada ya kufanya yenye urafiki na elimu wakati wote wa masomo yake.

Wakati akitafuta mambo yanayokubaliana na elimu anatakiwa ajiepushe kabisa na yale yanayo mfanya ashindwe darasani.

Mwanafunzi hazuiliwi kujiburudisha lakini inategemea sana na burudani anayoitumia kama inaurafiki na elimu.

MAPUMZIKO SALAMA

Mfano mwanafunzi badala ya kwenda beach na kukaa bure anaweza kufunga safari na kwenda sehemu za makumbusho na kufanya mapumziko yake hapo.Kwa kufanya hivyo anakuwa amepumzika pia ameongeza uelewa wa mambo ya kale.

Kwa wale wanaoishi karibu na hifadhi za kitalii wanaweza kutumiafursa hiyo kutembelea hifadhi hizo kwa gharama ambayo kila mmoja anamudu.

Wakati wa mapumziko marefu mwanafunzi anaweza kujiunga na shughuli mbali mbali za kiuzalishaji kwa ajili ya kujijengea uwezo wa kiuzalishaji baada ya kumaliza masomo .

Mfano mwanafunzi anaweza kujiunga kimafunzo katika shughuli ya ufugaji kuku wa kisasa,uchongaji wa vinyago,uchoraji,ushonaji,uhunzi,mapishi,kuendesha biashara za duka,genge,shughuli za stationary , huduma za internet nk.

Vilevile mwanafunzi anaweza kutumia muda wake wa likizo kutembelea shughuli za kiviwanda,kielimu kama vyuo mbalimbali,mahakama kusikiliza kesi,hospitalini kujionea wagonjwa na huduma zinazotolewa,kutembelea vituo vya watoto yatima,mashamba makubwa na madogo kujionea kilimo kinavyoendeshwa nk. katika maeneo yote hayo mwanafunzi anakuwa amepata uzoefu wa mambo mbalimbali kulingana na eneo husika.
Kwa kufuata mazingira yanayomjenga mwanafunzi siku zote atabaki salama na ufaulu wake kuongezeka siku baada ya siku.

Ni imani yangu kuwa kama tutazingatia hayo kiwango cha ufaulu kinaweza kuongezeka na kuzidi kile cha siku za nyuma hata bila kutumia gharama kubwa za kifedha kama wengine ambavyo tumekuwa tukifikiri.


Maoni 1 :