Jumanne, 15 Aprili 2014

MAMBO 5 YA KUFANYA KWANZA UFIKAPO CHUO AU SHULE

1.ONYESHA MSIMAMO WAKO KABLA WENZAKO HAWAJA KUONYESHA WA KWAO



Kufanya hivyo kutakusaidia kukutambulisha kuwa wewe ni mtu wa aina gani na unakubaliana na nini.Mara nyingi watakaokufahamu kwa mara ya kwanza watalazimika kufuata msimamo wako.

Wale wenye tabia ya utani,dhihaka,na mambo mengine ya masihara watajifikiria mara mbili kukuanza endapo watagundua kuwa wewe ni kinyume chake.Kuchelewa kuonyesha msimamo wako kutakufanya baadaye kuwa mtumwa wa kuanza kutengeneza msimamo mpya wakati wenzako watakapokuwa wameshazoea kukuonyesha misimamo yao.

2.KUWA TAYARI KUPOTEZA

Mara baada ya kuonyesha (consistence) yaani usiyebadilika unaweza kuingia katika janga la kupoteza baadhi ya vitu.Kitu cha kwanza utapoteza idadi kubwa ya watu watakaokuwa karibu na wewe.Hilo ni kutokana na watu wengi kupenda kuwa karibu na watu wenye misimamo rahisi .”Hata wewe bila shaka unapenda kuwa karibu na mtu anayekubaliana na wewe kwa kila kitu unachotaka au unachofanya”.Utakosa baadhi ya fursa kutokana na kuwa na idadi ndogo ya fans nk.Lakini hali hii itakusaidia kukuhakikishia kuwa kila anayekuja kwako iwe kwa urafiki au kivyovyote vile anakubaliana na msimamo wako.

2.USITAFUTE  MARAFIKI ACHA WAJE WENYEWE

Hapa naomba nisisitize kuwa,marafiki wa shule/chuo wa moja kwa moja (direct contact friends) sio kama marafiki wa facebook na twitter ambao unaweza kuwa nao hata maelfu na wasikusumbue. Hawa ni watu wanaokuona kwa uhalisia wako,wanafahamu kilakitu kuhusu wewe. Wanajua uwezo wako, udhaifu wako,siri zako,na mipango yako.Na kibaya zaidi si kila binadamu ni salama kwako.

Wapo wanaopenda wakutumie kwa faida zao na imekwisha.Wapo watakaotaka ufuate kila wanachotaka.Wapo wasiopenda kuona unamzidi kwa chochote.Kuna mambo lukuki ambayo hata wewe unayafahamu kuhusu binadamu.

Acha rafiki wa kweli aje mwenyewe.Rafiki wa kweli ni Yule anayekubaliana na hali yako halisi sio ya ki-Facebook na twitter.Kufanya hivyo kutakusaidia kuwa na rafiki ambaye hatokuwa mzigo,kero wala kikwazo katika safari yako.

3.JIWEKE MATAWI YA CHINI HATA KAMA UKO JUU

Heshima tamu ni ile unayoheshimiwa bila gharama yoyote.Ili kujipatia heshima ya kweli basi jifanye huna haja nayo ukiitaka umeipoteza.Kumbuka kuwa kila mtu anapenda kuheshimiwa.Na hakuna mtu anayepoteza muda wake kujenga heshima ya mtu mwingine.Kitendo cha kujifanya u matawi ya juu kitawafanya wenzako wajione si kitu.
 kwasababu hawatapenda kujiona si kitu wataichukia tabia yako,wakiichukia tabia yako watakuchukia hata wewe.Bila shaka umeshawahi kuona mtu anayestahili heshima lakini wala hakuna anaye mtetemekea.Wengi wao utagundua ni kutokana na tabia zao za kujifanya wako juu hata kama ni kweli wanauwezo.

4.SOMA  (STUDY) TABIA ZA WATU

Katika kipindi cha kwanza kabisa unatakiwa kusoma tabia za watu kabla ya kufanya nao chochote. Unaweza kufanya hivyo kwa kujaribu kuwasiliana na kila aliyekaribu nawe bila kuonyesha nia ya kuhitaji ukaribu.

Ni rahisi sana kuchukuliana na watu kama unafahamu tabia zao.Kufanya hivyo kutakusaidia kuwafahamu watu wasumbufu na wale wenye manufaa kwako.Wale wakorofi,wanafiki,wezi na tabia nyingine hatarishi utawatambua katika kipindi hiki.

Usipowatambua watu ni rahisi kukubadilisha au kukuingiza katika matatizo.Matatizo hayo yanaweza kuwa ni pamoja na kufukuzwa shule au chuo au hasara ambayo hutaweza kuirejesha.Matatizo hayo ni pamoja na ugomvi,wizi,ulevi,ulaghai na mengineyo.

5.KUWA MTULIVU KWA KILAKITU

Kipindi cha mwanzo watu kukutana katika mikusanyiko haswa ya kishule, huwa na kawaida ya kila mtu kutaka kuonyesha yeye ni nani.Pia katika kipindi hiki Kila mtu huwa na pilika pilika za hapa na pale haswa kwa wale wanaoishi katika maeneo ya hostel au kwenye nyumba za pamoja.Jitahidi kuvuka katika kipindi hiki bila kuchukuliwa na upepo wa pilika pilika hizi .

Kama utamudu kubaki katika utulivu huo itakusaidia kubaki na taswira ya aina moja tu ya elimu kichwani mwako.Fahamu kuwa kitendo cha kushughulika na mambo mengi hapa mwanzoni, kunaweza kuruhusu mambo mengine nje ya elimu kuanza kuchukua nafasi moja kwa moja katika ufahamu wako.Na endapo kama yatakuwa na nguvu ya kutosha basi,yanaweza kufanya swala la elimu kukaa katika nafasi ya pili.









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni